AMKA MTANZANIA
Ongea Na Kocha Dr. Makirita Amani
#NjiaYaUtajiri; Pata Pesa Ya 'Kafie Mbali' Na Fikiri Sahihi Kifedha.
0:00
-51:48

#NjiaYaUtajiri; Pata Pesa Ya 'Kafie Mbali' Na Fikiri Sahihi Kifedha.

Rafiki yangu mpendwa,

Ukitoa hewa ambayo tunapumua bure, kila kitu kwenye maisha yetu tunakipata kwa kutumia fedha. Na hata pale unapopata changamoto ya magonjwa, hiyo hewa ya bure nayo inakuwa gharama kubwa.

Licha ya fedha kuwa muhimu sana kwenye maisha ya kila mtu, bado watu wengi sana wamekuwa hawaweki juhudi kwenye kujiimarisha kifedha na kuwa na aina ya maisha ambayo wanayataka.

Wengi huona mambo ya fedha ni magumu kueleweka na wametingwa na majukumu yao mengine ya maisha. Lakini hivyo sivyo uhalisia ulivyo, mambo ya fedha binafsi ni rahisi na yanaeleweka kabisa.

Mwandishi J L Collins kwenye kitabu chake kinachoitwa THE SIMPLE PATH TO WEALTH ameshirikisha njia ya uhakika ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha na maisha ya uhuru na utajiri.

Kwenye kitabu hiki ameelezea kwa urahisi mno dhana ya USIMAMIZI WA FEDHA BINAFSI na kuweka mkazo zaidi eneo la uwekezaji ambalo watu huwa hawalielewi.

Karibu kwenye masomo haya ya kutoka kwenye kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ili ujifunze na kuchukua hatua kujiimarisha kifedha. Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu hicho, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

UTANGULIZI.

Fedha ndiyo zana kuu ya kuendesha maisha hapa duniani. Kuielewa fedha ni wajibu wa msingi wa kila mtu aliye hai.

Ukiweza kubobea kwenye fedha, inakuwa mtumwa wako na kukutumikia vyema. Lakini ukishindwa kubobea kwenye fedha, unakuwa mtumwa wa fedha na inakutumikisha sana.

Watu wengi wamekuwa wanashindwa kubobea kwenye fedha, kwa sababu tayari wana mambo mengi ya kuhangaika nayo kwenye maisha yao. Wana kazi au biashara za kufanya, wana familia za kulea na majukumu mengine.

Hilo limewaacha wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu fedha na matokeo yake kufanya maamuzi ambayo yamekuwa yanawagharimu sana.

MISINGI MUHIMU YA KIFEDHA.

Kuna mambo ya msingi kabisa kuhusu fedha ambayo kila mtu anapaswa kuyajua. Baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo;

1. Tumia chini ya kipato chako, wekeza, epuka madeni. Hii ndiyo kanuni kuu ambayo mtu yeyote akiifuata, atafanikiwa siyo tu kwenye fedha, bali kwenye kila eneo la maisha yake.

2. Fedha inatakiwa kukupa wewe uhuru wa kuyaishi maisha yako kwa namna unavyotaka mwenyewe.

3. Kufikia uhuru wa kifedha haraka, unapaswa kupambana uweze kuweka akiba nusu ya kipato chako na kuwekeza.

4. Soko la hisa ni nyenzo kuu ya kujenga utajiri, hakikisha unakuwa sehemu ya soko hilo.

5. Pale unapoweza kuishi kwa 4% ya uwekezaji wako kwa mwaka, umefikia uhuru wa kifedha.

HADITHI YA MTAWA NA WAZIRI.

Vijana wawili walikua pamoja tangu wakiwa watoto. Baada ya kuhitimu masomo, mmoja akawa mtawa na mwingine akawa waziri. Baada ya miaka mingi kupita, wakakutana, mtawa akionekana kuwa masikini asiye na kitu huku waziri akionekana kuwa tajiri anayejiweza.

Mazungumzo yao yakawa kama ifuatavyo;

WAZIRI; “Ukijifunza kumtumikia mfalme, hutalazimika kuishi kwa kula wali na maharage kila siku.”

MTAWA; “Ukijifunza kuishi kwa kula wali na maharage kila siku, hutalazimika kumtumikia mfalme”.

Watu wote tupo kati ya hao wawili, mwandishi anatushauri ni bora tuwe zaidi upande wa mtawa kuliko upande wa waziri.

SEHEMU YA KWANZA; MIONGOZO MUHIMU YA KIFEDHA.

Sehemu hii ya kwanza ya kitabu ina miongozo muhimu ya kifedha ambayo kila mtu anapaswa kuijua na kuizingatia ili aweze kujenga utajiri.

1. Deni ni mzigo usiokubalika.

Deni ni kaburi la utajiri na uhuru wa kifedha. Deni binafsi ndiyo kikwazo kikubwa kwa watu kuweza kujenga utajiri kwenye maisha yao. Hiyo ni kwa sababu madeni huwa yanalipwa kwa riba na kwa kuwa madeni binafsi huwa hayazalishi, riba ambayo mtu anailipa kwenye madeni ni fedha anakuwa amechagua kupoteza.

Madeni yamekuwa yanachukuliwa kama kitu cha kawaida kwa sababu yanatangazwa kwa njia mbalimbali. Wafanyabiashara wanatumia zaidi madeni kuwashawishi watu wanunue vile wanavyouza.

Kama upo kwenye madeni, kipaumbele cha kwanza kwako ni kuondoka kwenye madeni hayo. Na ukishaondoka kwenye madeni hakikisha haurudi tena.

Kuendelea na hatua nyingine yoyote ya kifedha kabla ya kuondokana na madeni ni kuendelea kujichimbia shimo kwa sababu riba ya madeni inakugharimu sana.

2. Unahitaji Pesa ya ‘KAFIE MBALI’.

Ili uweze kuwa huru kifedha, lazima uweze kuamua wewe mwenyewe ni NINI unafanya, unafanya LINI, unafanyia WAPI na unashirikiana na NANI. Kama huwezi kuamua yote hayo wewe mwenyewe bila ya kuomba ruhusa ya mtu mwingine, basi haupo huru kifedha.

Ili uweze kufikia uhuru huo, unahitaji kuwa na pesa ya ‘KAFIE MBALI’ (F- You Money). Hicho ni kiasi cha fedha ambacho ukiwa nacho unaweza kuacha kazi muda wowote unaotaka kwa sababu unaweza kuendesha maisha yako bila ya kutegemea kipato cha moja kwa moja.

Kiasi cha pesa cha kukupa uhuru huu siyo kikubwa sana, ukiwa na matumizi madogo na kuwa na uwekezaji ambao unakuzalishia kiasi cha kuweza kuyaendesha maisha yako, umefikia uhuru huo.

Kuishi kwa kutegemea kipato cha moja kwa moja ni utumwa. Kadhalika kuwa na madeni ni utumwa. Ukiweza kuondokana na hivyo viwili, umekuwa huru.

3. Kila mtu anaweza kutajirika, lakini siyo wote watafanya.

Kila mtu mwenye njia yoyote ile ya kuingiza kipato, anaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake. Lakini siyo wote watafanya, kwa sababu wengi hawana maarifa na wakiwa nayo hawana nidhamu ya kutosha kuchukua hatua ili kufikia utajiri.

Kanuni kuu ya kujenga utajiri ambayo inaweza kufanya kazi kwa mtu yeyote anayeifanyia kazi ni; MATUMIZI YASIZIDI KIPATO, WEKEZA NA EPUKA MADENI.

Yeyote anayeweza kufuata kanuni hiyo na akajipa muda wa kutosha, lazima atajenga utajiri.

Na kwa wale ambao hawataki kutumia miaka mingi sana, kama wakiweza kuweka akiba na kuwekeza nusu ya kipato chao, kati ya miaka 10 mpaka 15 wanakuwa wamefikia uhuru wa kifedha.

Hapa unakwenda kujifunza yote unayopaswa kujua na kufanya, wajibu wako ni kuchukua hatua.

4. Jinsi ya kufikiri kifedha.

Kuna ngazi tatu za kufikiri kifedha.

Ngazi ya kwanza ni fedha siyo tu kuhusu matumizi.

Wengi wanapopata fedha huwa wanafikiria tu matumizi na ndiyo maana fedha hazijawahi kutosha. Hatua ya kwanza unapaswa kuvunja hilo na kujua fedha siyo matumizi pekee.

Ngazi ya pili ni kufikiria fursa unazozipoteza pale unapotumia fedha.

Unapotumia fedha, siyo tu unaikosa hiyo fedha, bali pia unakosa faida ambayo ungeizalisha kama ungewekeza fedha hiyo vizuri. Kwa kufikiria hivi unaona jinsi ambavyo kutumia fedha inakugharimu.

Ngazi ya tatu ni kufikiri kwa usahihi kuhusu uwekezaji.

Uwekezaji huwa una tabia ya kupanda na kushuka, ili uweze kunufaika ni lazima uwe imara na uvumilie kupanda na kushuka huko.

5. Kuwekeza kwenye soko ambalo halijatulia.

Soko la hisa halijatulia, lina kupanda na kushuka kwa mara kwa mara. Watu wengi ambao hawana uelewa mzuri wa soko la hisa, wamekuwa wanaingia hasara mara zote.

Kinachofanya watu waingie hasara kwenye uwekezaji wa soko la hisa ni HOFU NA TAMAA. Pale hisa zinapopanda bei, watu wanaingiwa tamaa na kununua. Na pale hisa zinaposhuka bei, watu wanaingia hofu na kuuza.

Hivyo matokeo yanakuwa ni hasara, kwa sababu watu wananunua kwa bei ya juu na kuuza kwa bei ya chini.

Faida kwenye soko la hisa inapatikana kwa kuwekeza kwa muda mrefu na kuacha kuhangaika na hisia za muda mfupi. Kama ambavyo tutaendelea kujifunza kwenye kitabu hiki, kupanda na kushuka kwa soko la hisa ni kawaida. Lakini mwisho wa siku, soko huwa linapanda.

Ukiwa na utulivu, soko litapanda na utapata faida kwa muda mrefu.

Hapa tumepata sehemu ya kwanza ya kitabu ambayo imegusa yale ya msingi kuhusu usimamizi wa fedha binafsi. Kwenye masomo yanayofuata tutajifunza kuhusu uwekezaji kama njia ya kujenga utajiri.

Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu THE SIMPLE PATH TO WEALTH, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.

Discussion about this episode