AMKA MTANZANIA
Ongea Na Kocha Dr. Makirita Amani
#NjiaYaUtajiri; Tumia Mifuko Ya Pamoja Ya Uwekezaji Kujenga Utajiri Mkubwa.
0:00
-57:39

#NjiaYaUtajiri; Tumia Mifuko Ya Pamoja Ya Uwekezaji Kujenga Utajiri Mkubwa.

Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanaposikia kujenga utajiri kupitia uwekezaji, huwa wanaona haiwahusu. Hiyo ni kwa sababu wanakuwa na vipato vidogo na kudhani uwekezaji ni mpaka mtu uwe na kiasi kikubwa cha fedha.

Wengi wanaposikia uwekezaji wanawaza ardhi na majengo, au kama ni kwenye masoko ya mitaji basi hisa na hatifungani ambazo mtu anapaswa kuanza na kiasi kikubwa cha mtaji.

Lakini ukweli ni kwamba kwenye masoko ya mitaji, kuna aina mbalimbali za uwekezaji ambazo kila mtu anaweza kuzitumia kujenga utajiri kwenye maisha yake.

Na moja ya njia hizo ni mifuko ya pamoja ya uwekezaji.

Mifuko ya pamoja ya uwekezaji huwa inakusanya mitaji kutoka kwa wawekezaji wengi, kisha yenyewe inafanya uwekezaji kulingana na mipango yake.

Mifuko hiyo inakuwa na sera zake za uwekezaji pamoja na wataalamu wa uwekezaji wanaofanya maamuzi ya wapi uwekezaji ufanyike.

FAIDA ZA MIFUKO YA PAMOJA.

Mifuko hiyo ina faida mbalimbali, ambao baadhi ni;

1. Mtu kuweza kuwekeza kiasi kidogo kabisa ambacho huenda kisiwezekane kwenye aina nyingine za uwekezaji.

2. Mtu yeyote kuweza kuwekeza hata kama hana uelewa mkubwa kwenye uwekezaji.

3. Mtu kutokuhitajika kufuatilia sana mwenendo wa uwekezaji kwa sababu kuna wataalamu wanafanya hivyo.

4. Mtu kuweza kununua na kuuza uwekezaji muda wowote anaotaka na kutokulazimika kusubiri mpaka mteja apatikane.

5. Kupungua kwa hatari ya uwekezaji kwa sababu mifuko inatawanya sana uwekezaji wake.

SOMA; Mpango Binafsi Wa Uwekezaji Kupitia Mifuko Ya Pamoja Ya UTT AMIS.

CHANGAMOTO ZA MIFUKO YA PAMOJA.

Pamoja na faida hizo za mifuko ya pamoja, huwa pia ina changamoto zake. Baadhi ni;

1. Faida ndogo ukilinganisha na aina nyingine za uwekezaji, kwa sababu ya gharama za kuendesha mifuko na utawanyaji wa uwekezaji ambao unafanya marejesho yasiwe makubwa.

2. Mwekezaji kutokuwa na mamlaka ya kuamua wapi uwekezaji ufanyike au usifanyike.

3. Hatari ya kawaida kwenye kila uwekezaji ambayo huwa ipo.

Pamoja na changamoto hizo, bado mifuko ya pamoja ya uwekezaji ni njia nzuri ya kila mtu kutumia kujenga utajiri.

Hii ndiyo njia ambayo nimekuwa nashauri kila mtu anayeingiza kipato aitumie kuwekeza, ili apeleke umakini wake kwenye shughuli kuu ya kuingiza kipato na siyo kuhangaika na uwekezaji.

KARIBU KWENYE NGUVU YA BUKU.

Ili kuhakikisha wewe rafiki yangu unanufaika na fursa hii ya uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja, yaani unafanya kwa vitendo, nimekuandalia programu maalumu ya kujifunza na kuwekeza kwa vitendo.

Programu hiyo inaitwa NGUVU YA BUKU. Hii ni programu ambayo kila mshiriki anatenga angalau elfu moja ya kuwekeza kila siku na kwa wiki anawekeza kiasi kisichopungua elfu 7.

Ili kuwekeza kwa uhakika, kila mshiriki anapaswa kutuma ushahidi wa uwekezaji wake kwenye kundi. Ni programu ambayo inakupa uwajibikaji mkubwa kwenye kuwekeza kwa uhakika.

Kushiriki programu hii ni BURE, hakuna ada ya kuwepo. Unachohitaji ni kuwa na kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI pekee. Kama ungependa kuwa ndani ya programu hii, wasiliana sasa na namba 0678 977 007. Tuma ujumbe NGUVU YA BUKU kwenda kwenye hiyo namba na utapata maelekezo.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini, tumekuwa na mjadala mzuri sana kuhusu uwekezaji kwenye hiyo mifuko ya pamoja na hatua za kuanza kuchukua mara moja ili usijicheleweshe kwenye kujenga utajiri. Karibu ujifunze na kuchukua hatua ili kunufaika na uwekezaji huu ambao upo ndani ya uwezo wako kabisa.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.

Discussion about this episode