AMKA MTANZANIA
Ongea Na Kocha Dr. Makirita Amani
Kama Ndiyo Unaanza Uwekezaji, Anzia Hapa.
0:00
-1:20:00

Kama Ndiyo Unaanza Uwekezaji, Anzia Hapa.

Habari njema Matajiri Wawekezaji,

Karibuni kwenye mfululizo wa masomo yetu ya programu ya NGUVU YA BUKU, ambapo tunajifunza na kufanya uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo na kujenga utajiri kwa uhakika.

Kauli mbiu yetu kwenye NGUVU YA BUKU, ambayo pia ndiyo imani yetu ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hilo tuna uhakika nalo kwa sababu kwa fedha ndogo ndogo ambazo kila mtu anazipata, tukiziwekeza kwa muda mrefu kwa msimamo bila kuacha, tunaweza kujenga utajiri mkubwa.

Kwenye kundi la FAMILIA YA KISIMA CHA MAARIFA, ambalo ndiyo kundi mama la mafunzo yanayotolewa na Kocha Dr. Makirita Amani, tumekuwa na mijadala ya uwekezaji kwa ujumla.

Tunajadili aina zote za uwekezaji bila kuacha chochote. Ni kuanzia uwekezaji wa mifuko ya pamoja (vipande), hisa, hatifungani, mali n.k. Mijadala hiyo imekuwa ni ya kujifunza na kushirikishana kutoka kwenye kufanya uwekezaji kwa vitendo.

Mijadala hiyo imekuwa inaibua shauku kwa wengi kutaka kujifunza kwa kina zaidi na kufanya uwekezaji. Na uwekezaji ambao watu wamekuwa wanapenda sana kujifunza na kufanya ni kwenye SOKO LA HISA na HATIFUNGANI.

Tunapouliza kujua kama watu hao wameshaanza kufanya uwekezaji wowote, majibu yanakuwa ni bado hawajaanza kabisa.

Hivyo nimeandaa mwongozo huu wa uwekezaji kwa watu wote, hasa ukiwalenga ambao ni wageni ili waweze kujua mahali sahihi pa kuanzia kwenye safari ya uwekezaji.

SOMA; Mpango Wa Usimamizi Wa Fedha Binafsi (Personal Finance Management Plan)

Karibu ujifunze na uwashirikishe wengine mwongozo huu ili waweze kufanya maamuzi sahihi.

UWEKEZAJI NI NINI?

Uwekezaji ni kuifanya fedha ikufanyie wewe kazi. Yaani uweze kutumia fedha zako kuzalisha fedha zaidi bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.

KWA NINI UWEKEZE?

Ni muhimu kuwekeza kwa sababu kadiri umri wako unavyokwenda, nguvu za wewe kufanya kazi zinapungua wakati mahitaji yanaongezeka. Hivyo ni lazima uweze kuingiza kipato cha kuendesha maisha yako bila kufanya kazi moja kwa moja.

NINI MALENGO YA UWEKEZAJI?

Malengo ya uwekezaji ni kufikia UHURU WA KIFEDHA. Na uhuru wa kifedha ni pale unapoweza kuyaendesha maisha yako bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Yaani uweze kuingiza kipato cha kutosha kuendesha maisha yako hata kama hufanyi kazi. Na hilo utalifikia kupitia uwekezaji.

KUNA AINA NGAPI ZA UWEKEZAJI?

Uwekezaji umegawanyika kwenye makundi mbalimbali, hapa tutaangalia aina kuu ambazo tumekuwa tunajadiliana mara kwa mara;

1. Uwekezaji kuputia mifuko ya pamoja. Hapa mfuko unakusanya mitaji kwa wawekezaji na kwenda kuwekeza kisha unarudisha faida kwa wawekezaji.

2. Uwekezaji kwenye soko la hisa. Hapa unachangia mtaji kwenye kampuni na inapopata faida unapata gawio. Pia kukua kwa thamani ya kampuni na hisa kunakupa faida.

3. Uwekezaji kwenye hatifungani. Hapa unaikopesha serikali au taasisi fedha na yenyewe inakulipa riba kwa kipindi chote cha makubaliano. Mwisho unarudishiwa kile kiasi ulichowekeza.

UWEKEZE KIASI GANI?

Kiasi cha kuwekeza kinaamuliwa na malengo yako. Lakini kuna kanuni kuu mbili tunazofuata;

Moja ni MWENDOPOLE; Hapa unawekeza angalau asilimia 10 ya kipato chako. Njia hii itakuchukua miaka 20 mpaka 30 kufikia uhuru wa kifedha, kulingana na kipato chako na gharama za maisha.

Mbili ni MWENDOKASI; Hapa unawekeza angalau asilimia 50 ya kipato chako. Njia hii inakuchukua miaka 10 mpaka 15 kufikia uhuru wa kifedha, kulingana na kipato na gharama.

Unaweza kuwa pia na mseto wa njia hizo kulingana na vipindi mbalimbali unavyopitia kwenye maisha.

UWEKEZE WAPI?

Watu wengi huwa wanavutiwa kwenye uwekezaji na vitu vinavyosisimua, mfano kuwekeza na kupata faida kubwa na ya haraka. Lakini ukweli ni uwekezaji sahihi huwa hausisimui, badala yake unaboa.

Uwekezaji unaboa kwa sababu inachukua muda mrefu kuweza kuiona faida kubwa ya uwekezaji, tofauti na njia nyingine za kuingiza kipato kama kuajiriwa, kujiajiri au kufanya biashara.

Hivyo kigezo cha kwanza kwenye kuchagua uwekezaji ni kuepuka uwekezaji wowote unaosisimua sana, kwa sehemu kubwa utakusumbua sana au kukupa hasara kabisa.

SOMA; Jinsi Ya Kujenga Utajiri Wa Mwendokasi.

USHAURI KWA ANAYEANZA KABISA.

Kwa mtu ambaye ndiyo anaanza uwekezaji, sehemu sahihi ya kuanzia ni UWEKEZAJI WA MIFUKO YA PAMOJA. Kwa Tanzania ipo mifuko minne mpaka sasa ambayo ni UTT AMIS, FAIDA, TIMIZA na SANLAM.

Sababu za kuanza na mifuko ya pamoja ni;

1. Ni rahisi kuwekeza, huhitaji kufanya mchakato wowote mrefu kuwekeza. Naweza kuwekeza popote ulipo bila kuathiri shughuli zako.

2. Unaweza kuwekeza kiasi kidogo kabisa ambacho unaweza kumudu.

3. Huhitaji kujua chochote kuhusu uwekezaji, kwa sababu waendeshaji wa mifuko wana wataalamu wa uwekezaji wanaofanya kazi kubwa.

4. Uwekezaji wako hauathiri shughuli zako nyingine unazofanya, kwa sababu huhitaji kufuatilia sana mwenendo wa uwekezaji.

5. Ni rahisi kutoa uwekezaji wako na kupata fedha pale unapohitaji, kwa sababu husubiri mpaka mteja apatikane ndiyo uuze, bali mfuko unanunua uwekezaji wako na kukupa fedha.

Katika mifuko iliyopo sokoni kwa sasa, ni vyema kuanza na mifuko ya UTT AMIS kwa sababu;

1. Imekuwepo kwa muda mrefu, karibu miaka 20 sasa, hivyo ni kiashiria ina uwezo wa kuendelea kufanya vizuri.

2. Ina mifuko mingi ndani yake, inayoendana na mahitaji mbalimbali ambayo mtu unakuwa nayo. UTT AMIS wana mifuko sita ambayo ni UMOJA, WATOTO, WEKEZA MAISHA, JIKIMU, UKWASI na BOND.

3. Unaweza kufungua, kuwekeza na kuuza uwekezaji wako kwa kutumia simu yako ya mkononi bila ya kulazimika kwenda mbali ndiyo ukakamilishe hayo.

4. Mfuko unasimamiwa na serikali na una wadhamini nje ya serikali hivyo kuufanya kuwa salama zaidi.

5. Ukuaji endelevu wa mifuko kila mwaka umekuwa unatoa rejesho zuri na la uhakika kwa wawekezaji.

KWA NINI UEPUKE HISA NA HATIFUNGANI KAMA NDIYO UNAANZA?

Katika aina zote za uwekezaji, uwekezaji wa hisa ndiyo wenye faida kubwa zaidi kuliko zote, kwa muda mrefu. Na uwekezaji wa hatifungani ndiyo ulio salama zaidi kuliko aina nyingine.

Lakini kama ndiyo unaanza uwekezaji, au bado kiasi unachowekeza ni kidogo, ni vyema usijihusishe na uwekezaji wa hisa na hatifungani kwanza. Hiyo ni kwa sababu zifuatazo;

1. Uwekezaji wa hatifungani unataka kiwango cha chini cha Tsh Milioni moja kwa wakati mmoja, kiasi ambacho kama unaanza unaweza usiwe nacho.

2. Uwekezaji wa hisa unahitaji uwe na ufuatiliaji wa mwenendo wa soko ili kufanya maamuzi sahihi. Hiyo ni kazi ya ziada, hasa pale unapokuwa na majukumu mengine tofauti na uwekezaji.

3. Uwekezaji kwenye hisa unahitaji utawanyaji mkubwa ili kupunguza hatari ya kupoteza pale aina fulani ya hisa inapofanya vibaya. Kama mtaji wako ni mdogo huwezi kufanya utawanyaji mzuri.

Kwa sababu hizi na nyingine zinazoendana na hizo, unapoanza usiingie kwanza kwenye hisa na hatifungani, bali anza na mifuko ya pamoja, ambayo ndiyo inaenda kuwekeza huko.

NI WAKATI GANI WA KWENDA KWENYE HISA NA HATIFUNGANI?

Ieleweke kwamba siyo hutawekeza kabisa kwenye hisa na hatifungani, huko utafika baadaye. Lakini kwanza jifunze uwekezaji na jenga mtaji kupitia uwekezaji wa mifuko ya pamoja ili pia uweze kuendelea na shughuli zako nyingine za kukuingizia kipato.

Utaweza kuingia kwenye uwekezaji wa hisa na hatifungani ukishakuwa una uelewa wa msingi kuhusu uwekezaji na jinsi unavyofanya kazi, pamoja na kuwa umeshajenga mtaji wa kutosha kufanya uwekezaji utakaokupa faida na marejesho mazuri.

Japo pia siyo lazima uingie kwenye hisa na hatifungani moja kwa moja, kama mifuko ya pamoja inakupa faida inayokutosha, utulivu mkubwa ambao unaupata kwa kuwekeza kwenye mifuko hiyo ni faida kuliko faida ya ziada ambayo ungeipata kwa kwenda sokoni moja kwa moja.

HATUA ZA KUCHUKUA.

Baada ya kujifunza haya, chukua hatua zifuatazo mara moja ili uanze kunufaika kupitia uwekezaji;

1. Jiunge na programu ya NGUVU YA BUKU ambayo inatoa mafunzo, mwongozo na usimamizi wa kufanya uwekezaji kwa msimamo bila kuacha.

2. Fuata maelekezo yanayotolewa kwenye programu ya NGUVU YA BUKU, kwa kufungua akaunti ya uwekezaji ya UTT AMIS na kuwekeza kila wiki kisha kutuma ushahidi wa uwekezaji wako.

3. Endelea kujifunza kuhusu uwekezaji kupitia programu ya NGUVU YA BUKU na njia nyingine ili uendelee kuwa na uelewa na kukuza pamoja na kutawanya uwekezaji wako.

SIKILIZA SOMO HILI KWENYE ONGEA NA KOCHA.

Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala mzuri wa somo hili ambapo washiriki wamekuwa na maswali na michango mbalimbali. Karibu usikilize hapo juu ili ujifunze na kuchukua hatua sahihi.

MJADALA WA SOMO.

Karibu kwenye mjadala wa somo hili, shiriki kwa kutuma majibu ya maswali haya;

1. Kama ndiyo unaanza uwekezaji, unakwenda na mpango gani? Kama tayari unawekeza ila unataka kumshauri mtu wako wa karibu, utampa mpango gani wa uwekezaji ambao utamnufaisha?
2. Nje ya uwekezaji wa mifuko ya pamoja, ni uwekezaji upi mwingine ambao unapanga kufanya au umeshaanza kufanya? Unaufanya kwa mpango gani?

3. Umeielewaje dhana ya uwekezaji unaosisimua na unaoboa? Unatumiaje dhana hiyo kupima usahihi wa uwekezaji kabla ya kuingia?

4. Ni vigezo vipi umejiwekea katika kuingia kwenye uwekezaji mwingine kwa ukubwa ukiacha uwekezaji kwenye mifuko ya pamoja?

5. Karibu kwa maswali, maoni, mapendekezo na shuhuda kuhusu somo hili na programu nzima ya NGUVU YA BUKU na UHURU WA KIFEDHA.

Tuma majibu ya maswali hayo kama uthibitisho wa kusoma, kuelewa na kutekeleza somo hili la uwekezaji.

Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,

Kocha Dr. Makirita Amani,

Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi

+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com

www.amkamtanzania.com

MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.

Discussion about this episode