Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanakosa utulivu kwenye maisha yao kwa sababu akili zao zinakosa busara.
Wanajikuta wakihangaika na mambo mengi ambayo hayana tija kwao na kuishia kuchoka sana na wasipate matokeo mazuri.
Mwanafalsafa wa Ustoa Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha 11 Meditations alishirikisha tabia za akili yenye busara. Hizo ni tabia ambazo zinampa mtu utulivu mkubwa wa kuweza kuyaishi maisha yake kwa tija.
Tabia Ambazo Marcus Aliziainisha Ni Kama Ifuatavyo;
Moja; Kuzama Ndani Yake Yenyewe.
Akili yenye busara huwa inazama ndani yake yenyewe badala ya kuhangaika na mambo ya nje. Ndani ya kila akili kuna vitu vingi ambavyo mtu akiweza kuvielewa na kuvibobea, ataweza kufanya makubwa kwenye maisha yake. Lakini wengi wamekuwa wanaenda kinyume, wanahangaika na mambo ya nje na kuacha uimara ulio ndani yao.
Mbili; Kupenda Matunda Yake Yenyewe.
Mtu kupenda matunda ya kazi yake ni busara ya hali ya juu. Kama huwezi kupenda kile unachofanya na matokeo unayopata, huwezi kuleta matokeo makubwa na mazuri. Ni kupitia kupenda unachofanya na unachopata ndiyo unaweza kufanya kwa ubora wa hali ya juu. Hayo yote yapo ndani ya uwezo wa mtu kuyafanyia kazi kwa uhakika.
Tatu; Kuwa Imekamilisha Lengo Lake Kwenye Kila Wakati.
Katika kila wakati, mtu unapaswa kuwa umekamilisha kila unalokuwa umepanga. Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wamekuwa ni wazuri wa kuahirisha mambo wanayopanga. Matokeo yake ni kila wakati kuwa na mambo ambayo wanapaswa kukamilisha ila bado hawajafanya hivyo. Hakikisha kila wakati unakua umekamilisha yale uliyopanga. Unapoimaliza siku, hakikisha umekamilisha yale uliyopanga kwenye siku hiyo. Ni kwa kwenda hivyo ndiyo unaweza kukabiliana na maisha kwa namna sahihi.
SOMA; Falsafa Ya Ustoa; Maisha Mazuri Yapo Kila Mahali.
Nne; Kutambua Mzunguko Wa Dunia.
Dunia ina mzunguko ambao huwa unajirudia. Hakuna ambacho ni kipya kabisa hapa duniani, ni mambo yale yale yamekuwa yakijirudia. Akili yenye busara huwa inaelewa mzunguko huu wa dunia na haikubali kusumbuliwa na hilo. Hata kama mambo yanaonekana kuwa na changamoto kiasi gani, wanakuwa wanajua ni swala la muda tu, mambo yatabadilika. Hakuna kinachobaki vile kilivyo, kila kitu kinabadilika, lakini pia mabadiliko yanakuwa ni ya kujirudia.
Tano; Kumpenda Jirani.
Akili yenye busara inajua kwamba haiwezi kujitosheleza kwa kila kitu, hivyo inategemea sana ushirikiano na watu wengine. Hilo ndiyo linafanya kuwapenda wanaotuzunguka kuwa hitaji muhimu kwenye maisha yetu. Unawahitaji sana watu wengine ili uweze kupiga hatua unazotaka hivyo kuwapenda ni hatua muhimu ya kuweza kushirikiana nao vizuri.
Hizo ndizo tabia unazopaswa kujijengea kama unataka kuwa na busara na kuyaendesha maisha yako kwa mafanikio makubwa. Kwa tabia hizo unakuwa na utulivu binafsi na kuweza kushirikiana vizuri na watu wengine.
Katika kumalizia somo hili, kuna kitu kimoja ambacho Marcus amekieleza kwenye kitabu ambacho ni muhimu sana tukielewe na kukiishi. Anasema; “Hakuna wakati mzuri wa kuishi falsafa kama huo ambao unapitia sasa.” Hii ni kauli yenye ujumbe muhimu sana, kwa sababu wote tuna falsafa na misingi mbalimbali, lakini huwa hatuitumii kwa usahihi. Kwa lolote unalokuwa unapitia kwenye maisha yako, ni fursa ya wewe kutumia falsafa na misingi yako kuvuka au kufanya vizuri zaidi. Usilalamikie tena yale unayopitia, badala yake tumia falsafa na misingi kukabiliana nayo.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini tumekuwa na mjadala mzuri kuhusu somo hili la falsafa ya Ustoa. Fungua ujifunze na kuweka unayojifunza kwenye vitendo ili uwe na maisha bora na tulivu.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
Share this post