Mrejesho Wa Siku Ya Kuzaliwa Ya Kocha Dr. Makirita Amani.
Rafiki yangu mpendwa,
Tarehe 28 mwezi Mei ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu. Katika kuiendea siku hiyo huwa natenga muda wa kutafakari kwa kina maisha yangu, kwa kuangalia nilikotoka, nilipo sasa na kule ninakokwenda.
Lakini pia huwa natumia fursa hiyo kuomba mrejesho kutoka kwenu marafiki zangu ambao ndiyo mnapokea kazi hizi ninazofanya. Napenda kusikia kutoka kwenu ni maeneo gani ya kuboresha zaidi ili kila anayefuatilia huduma hizi aweze kunufaika.
Hapo chini nimeshirikisha yale ya msingi kutoka kwenye tafakari ya kumbukizi ya siku yangu ya kuzaliwa na mrejesho kutoka kwenu marafiki zangu.
1. Historia Ya Huduma Kwa Ufupi.
Huduma ninazotoa zinaongozwa na kusudi na falsafa.
Kusudi linaloniongoza ni; KUYAFANYA MAISHA YA WENGINE KUWA BORA ZAIDI KUPITIA KILE NINACHOFANYA. Kiu yangu ni kuona kila anayekutana na kazi zangu, habaki vile alivyokuwa.
Falsafa kuu inayoniongoza ni; NAWEZA KUPATA CHOCHOTE NINACHOTAKA KAMA NITAWASAIDIA WENGINE WENGI KUPATA KILE WANACHOTAKA. Nina malengo makubwa mawili ninayoyafanyia kazi, kuwa bilionea na kuwa raisi wa Tanzania. Ili nifikie malengo hayo, nawajibika kuwasaidia watu wengi zaidi kupata yale wanayotaka. Na wewe ni mmoja wa hao, nimejitoa kuhakikisha nakusaidia kupata unachotaka ili na mimi nipate ninachotaka.
2. Kupenda Kusoma.
Nimekuwa napenda sana kusoma tangu nipo shule ya msingi. Nilikuwa nikisoma vitabu mbalimbali vya shuleni. Nikiwa darasa la tano niliweka lengo la kusoma biblia yote na kuimaliza, nilifanikiwa kumaliza agano la kale lote.
Hapo nilikuja kugundua moja ya uimara wangu ni kwenye kupenda kusoma na kuelewa vizuri na haraka kwenye usomaji. Na ndiyo maana sehemu kubwa ya huduma zangu inahusisha usomaji wa vitabu.
3. Kupenda Utajiri.
Nimezaliwa na kukulia kwenye familia ya chini kabisa. Lakini tangu nikiwa mtoto nilikuwa nasema nitakuja kuwa tajiri. Nakumbuka siku moja nilimwambia mama yangu kwenye haya maisha nitakuja kuwa tajiri, kwa namna yoyote ile. Nilikuwa mdogo sana na alinijibu ni utoto tu unanisumbua.
Hili limekuwa lengo langu ambalo ndiyo linanisukuma mpaka sasa, na sasa siyo ule utajiri wa kawaida ambao ni rahisi kufikia, bali ni utajiri wa ngazi ya ubilionea, ambao ni mkubwa sana na siyo rahisi kufikia. Lakini napambana na nina uhakika nitafikia.
4. Kuweka Na Kufikia Malengo.
Kwa kipindi chote cha maisha yangu, nimekuwa naweka na kufikia malengo. Nikiwa kidato cha tatu niliweka lengo la ufaulu wa daraja la kwanza kidato cha nne kwa kupata alama A tano, nilipata 4 na kuwa ufaulu wa juu zaidi kwenye shule hiyo. Nikiwa kidato cha tano, niliweka lengo la ufaulu wa daraja la kwanza kidato cha sita kwa kupata alama A zote na nilifikia. Hii ni mifano michache, mikubwa na ya wazi, ipo mingine mingi.
Hili limekuwa linanipa nguvu ya kuweka malengo makubwa na kuyapambania mpaka kuyafikia. Ndiyo maana nimekuwa sina wasiwasi na malengo makubwa ninayojiwekea, kwa sababu kila malengo niliyoweka na kuyafikia, yananipa nguvu zaidi.
5. Kufukuzwa Chuo.
Disemba 15 mwaka 2011 nilifukuzwa chuo nikiwa mwaka wa tatu wa mafunzo ya udaktari. Tukio hilo lilionekana kuvunja ndoto zote nilizokuwa nazo za kusoma, kufaulu na kupata kazi kama daktari. Baada ya kukaa mtaani kwa muda mfupi, nilijiambia kwamba kwenye maisha yangu nitapata mafanikio makubwa, iwe nina digrii au sina digrii. Na hapo ndipo nilipoanza kujifunza na kuchukua hatua mpaka kufikia hiki ninachofanya sasa.
Hili linaonyesha jinsi ambavyo changamoto unazokutana nazo kwenye maisha unaweza kuzitumia kupiga hatua zaidi badala ya kukubali zikukwamishe.
6. Kupambana Mtaani.
Baada ya kufukuzwa chuo na kuingia mtaani nikiwa sina digrii ambayo ndiyo kiashiria kwamba umesoma, ilinibidi kufanya kila aina ya kazi halali ili kuingiza kipato. Ni katika kipindi hicho ndiyo nilijifunza vitu vingi sana peke yangu, kuanzia kutengeneza blog, website, programu za kompyuta, uandishi na mengine mengi. Katika kujifunza mambo mengi ndiyo nilijikuta napenda zaidi upande wa kusoma, kuandika na kufundisha.
Hapa tunaona jinsi ambavyo nguvu ya kujifunza inaweza kumsaidia mtu kufanya chochote anachotaka. Hata kama huna vyeti vya kuhitimu elimu, ukiwa tayari kujifunza na kufanyia kazi unayojifunza unaweza kupiga hatua.
7. Kurudi Na Kumaliza Chuo.
Baada ya miaka mitatu niliweza kurudi chuoni na kumaliza masomo yangu ya udaktari na kutunukiwa shahada ya udaktari wa binadamu. Niliweza kurudi chuoni na kuendelea na masomo huku pia nikiendelea na shughuli nilizokuwa nimeanza kufanya, ikiwepo uandishi na biashara. Licha ya masomo ya udaktari kuwa magumu, niliweza kufanya vyote na kupata ufaulu mkubwa.
Hapa tunaona jinsi ambavyo mtu unaweza kufanya kazi au masomo na kuendesha shughuli nyingine za pembeni. Ukiweza kupangilia muda wako na mambo yako vizuri, unaweza kufanya mengi zaidi ya ilivyozoeleka.
8. Historia Ya Huduma;
Huduma ya mafunzo na usimamizi ninayotoa, imepitia vipindi mbalimbali kama ifuatavyo;
-AMKA MTANZANIA
Ilianza mwezi Machi mwaka 2013, nimekuwa naandika makala za maendeleo binafsi huko kila siku. Mtandao huo ni bure na utabaki kuwa bure.
-KISIMA CHA MAARIFA
Ilianza Januari 2014, kama sehemu ya watu kujifunza zaidi baada ya kujifunza kwa kiasi kwenye AMKA MTANZANIA. Ilikuwa ni huduma ya kulipia, ila kwa sasa haina tena malipo.
-SEMINA ZA MWAKA
Hizi zilianza Oktoba mwaka 2016 na tumekuwa nazo kila mwaka bila kukosa. Hizi ni semina za kukutana ana kwa ana, ambazo tumezifanya Dar es salaam, Dodoma, Arusha na Mbeya.
-KLABU ZA KISIMA CHA MAARIFA
Hizi zilianza mwaka 2019 ikiwa ni sehemu ya wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA walio ndani ya mkoa mmoja kuweza kukutana. Klabu zimekuwa na msaada mkubwa kwa wengi kuwajibika kwenye kuchukua hatua kwa yale tunayojifunza.
-VITABU
Nilianza kuandika vitabu mwaka 2014 vikiwa kama nakala tete (softcopy) na baadaye mwaka 2016 nilianza kuvichapa kama nakala ngumu (hardcopy). Mpaka sasa nimeandika vitabu zaidi ya 20 na vingi zaidi vinakuja.
-GAME CHANGERS
Hii ilikuwa huduma ya kuleta mabadiliko makubwa kwa mtu ndani ya mwezi mmoja. Huduma hii imewasaidia watu kubadili kabisa mtazamo wao na kuanzisha vitu vipya ndani ya muda mfupi. Huduma hii kwa sasa haipo tena.
-LEVEL UP
Hii ilikuwa huduma ya kukuza biashara kwenda ngazi ya juu zaidi. Huduma iliwasaidia watu kukuza biashara zao zaidi. Kwa sasa pia haipo.
-PERSONAL COACHING
Hii ilikuwa huduma ya kumsimamia mtu kuleta mabadiliko anayotaka kwenye maisha yake. Iwe ni kubadili tabia, kuanza kitu kipya n.k. Huduma hii imewawezesha watu kuandika vitabu, kuanza biashara na kukamilisha mipango mbalimbali. Huduma hii haipo tena.
MUHIMU; Kwa huduma ambazo hazipo tena, manufaa yake yapo kwenye huduma za juu zaidi zinazopatikana kwa sasa.
-CHUO CHA MAUZO
Hii ni huduma ya mafunzo ya mauzo kwa watu wote wanaofanya mauzo, kuanzia wamiliki wa biashara mpaka wafanyakazi wa mauzo. Huduma hii kwa sasa ndiyo inabeba mafunzo yote ya biashara kwa ngazi ya chini, ikiweka mkazo kwenye kujenga timu na kukuza mauzo.
-BILIONEA MAFUNZONI
Hii ndiyo huduma ya juu kabisa ya mafunzo na usimamizi kwenye kujenga na kukuza biashara inayojitegemea yenyewe. Washiriki wa huduma hii wanapata mafunzo ya juu kabisa ya kukuza biashara kwa ngazi ya kujitegemea.
-NGUVU YA BUKU
Hii ni huduma ya mafunzo na usimamizi kwenye uwekezaji kwa kufanya kwa hatua ndogo ndogo. Kwenye huduma hii, kiwango cha chini cha kuwekeza ni elfu 7 kila wiki, ila mtu anaweza kwenda zaidi ya hapo. Huduma hii tuna lengo la kufanya uwekezaji kwa miaka 10 kwa mfululizo bila kuacha. Tumeanza mwaka 2024 tutakwenda mpaka mwaka 2033/34.
-UHURU WA KIFEDHA
Hii ni huduma ya juu ya uwekezaji kwa wale ambao wanataka kufikia uhuru wa kifedha kwa uhakika. Kwenye huduma hii unasimamiwa kufanya uwekezaji ambao utakufikisha kwenye uhuru wa kifedha kwenye muda unaohitajika kulingana na hali ya mtu na lengo alilonalo.
9. Huduma za sasa;
Kwa sasa huduma zimeboreshwa kwa namna ambayo kila mtu anaweza kunufaika nazo. Baadhi ya huduma zilikuwa na gharama kubwa huko nyuma, ambapo kwa sasa zimeondolewa ili ziwanufaishe wengi zaidi.
Huduma kwa sasa zipo kama ifuatavyo.
-MAARIFA YOTE BURE; AMKA, KISIMA, TELEGRAM, YOUTUBE.
Kwa sasa maarifa yote ninayotoa ni bure. Kuna makala za kila siku kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA, kuna huduma ya KISIMA CHA MAARIFA, kuna vipindi vya ONGEA NA KOCHA telegram na youtube na yote hayo ni bure kabisa.
-VITABU
Vitabu vinapatikana kwa nakala tete ambavyo vinaanzia Tsh elfu 5 na nakala ngumu ambavyo vinaanzia Tsh elfu 20.
-NGUVU YA BUKU
Huduma hii haina gharama, unachohitaji ni kuwa na kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI. Kwa miaka yote 10 utakayosimamiwa kufanya uwekezaji, hautaingia gharama yoyote ya ziada. Ni wewe tu ufanye uwekezaji ili kuwa na sifa za kubaki kwenye huduma.
-CHUO CHA MAUZO
Huduma hii ina ada za kila mwezi kwa kila mshiriki.
-BILIONEA MAFUNZONI
Hii ina ada za kila mwezi kwa biashara nzima inayokuwa kwenye huduma.
-UHURU WA KIFEDHA
Hii ina gharama ya kila mwezi kwenye kusimamiwa kufanya uwekezaji mkubwa.
10. Mapendekezo yaliyotolewa sana;
Kwenye kutafakari siku yangu ya kuzaliwa, niliomba maoni ya maboresho kutoka kwenu. Mapendekezo mengi mazuri yametolewa, lakini matatu yamekuwa yanajirudia rudia sana.
-Kufikia wengi zaidi.
Hili ni pendekezo lililotolewa na wengi zaidi na ni kweli kabisa. Huduma ni nzuri lakini haijaweza kuwafikia wengi. Hivyo tunakwenda kuweka kazi kubwa hapa kuwafikia watu wengi zaidi.
-Gharama kubwa za huduma.
Mrejesho mwingine ulikuwa ni gharama kubwa za huduma. Na hili limeshafanyiwa kazi kwani huduma nyingi kwa sasa ni bure kabisa na nyingine zina gharama kidogo. Zimebaki huduma chache ambazo ada yake iko juu, kama BILIONEA MAFUNZONI na UHURU WA KIFEDHA, ambapo ukitumia vizuri huduma za chini, utaweza kumudu.
-Maboresho endelevu.
Imependekezwa pia huduma ziendelee kuboreshwa kulingana na mabadiliko na mahitaji ya watu. Na hili ndiyo umekuwa msingi mkuu wa huduma hizi. Ukiangalia mabadiliko ya hapo juu, yote ni lengo la kuboresha zaidi. Hivyo tutaendelea kuboresha.
11. Ombi langu kwako;
Rafiki, baada ya hayo yote nina maombi kwako kwenye ushiriki wako kwenye hizi huduma.
-Shiriki kikamilifu.
Naomba ushiriki kikamilifu kwenye huduma unazochagua. Usifurahie tu kujifunza, bali chukua hatua na uweze kunufaika.
-Waambie wengi zaidi.
Tunahitaji kuwafikia watu wengi zaidi kwa huduma hii. Na wewe ni mdau muhimu kwenye hili. Naomba tusaidiane kusambaza maarifa haya kwa wengi zaidi. Mengi ni bure kabisa na kila mtu anaweza kunufaika.
-Kuwa mfano mzuri.
Anza wewe kuwa mfano mzuri kwa wale wanaokuzunguka kwa kufanyia kazi yale unayojifunza. Watu wanapokutana na wewe wakuone ni wa tofauti na kutaka kujua siri yako. Hapo utawashirikisha huduma hizi na wao kuwa tayari kushiriki ili wawe bora.
-Kuwa kwenye NGUVU YA BUKU.
Kauli mbiu ya huduma ya NGUVU YA BUKU ni KILA MTU ANAWEZA KUWA TAJIRI. Hivyo kama unayapata maarifa ninayoyatoa, naomba uwe kwenye programu ya NGUVU YA BUKU. Kila mtu anaweza kutenga elfu moja kwa siku kwa ajili ya kuwekeza. Kwa pamoja nataka tutengeneze historia mpya kwenye taifa letu, kwa kufanya uwekezaji kidogo kidogo kwa muda mrefu na kujenga utajiri mkubwa. Karibu uwe sehemu ya historia hii ya kipekee.
-Mawazo ya maboresho zaidi.
Naomba uendelee kutoa mawazo ya maboresho zaidi ya huduma hizi. Kadiri unavyopokea hizi huduma, mawazo yoyote ya kuboresha unayokuwa nayo, usisite kushirikisha. Tutaendelea kupokea mawazo hayo na kuyafanyia kazi kadiri inavyofaa.
Shukrani za dhati.
Nichukue nafasi hii kukushukuru tena kwa kuwa sehemu ya ukuaji wa hii huduma. Bado ninakuhitaji sana kwenye ukuaji zaidi. Lengo langu ni kukuwezesha wewe kupata unachotaka, ili na mimi niweze kupata ninachotaka.
Hapo chini ni kipindi cha ONGEA NA KOCHA ambapo nimeyaeleza haya yote kwa ufafanuzi zaidi na baadhi ya washiriki kuweza kutoa mirejesho yao kulingana na walivyonufaika na huduma na pia kutoa mawazo ya kuboresha zaidi. Karibu usikilize kipindi na kuweza kuchukua hatua sahihi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
Share this post