Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu ambaye ana shughuli yoyote ya kumwingizia kipato, anaweza kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yake.
Unaweza kushtushwa na kauli hiyo, hasa ukizingatia jinsi watu wengi wenye shughuli za kuwaingizia kipato wanavyobaki kwenye umasikini.
Lakini huo ni ukweli, ambao ukiuelewa na kuufanyia kazi, utaweza kujenga utajiri na uhuru wa kifedha kwenye maisha yako.
Mwandishi J L Collins kwenye kitabu chake kinachoitwa THE SIMPLE PATH TO WEALTH ameshirikisha njia ya uhakika ya kuelekea kwenye uhuru wa kifedha na maisha ya uhuru na utajiri.
Kwenye kuhitimisha kitabu chake, mwandishi ameshirikisha mpango wa miaka 10 ya kwanza ya mtu kwenye kujenga utajiri. Kwenye kipindi hicho ameshirikisha mambo muhimu ya kuzingatia kama ifuatavyo;
1. Epuka madeni. Kulipa riba kwenye madeni ni kaburi la utajiri.
2. Epuka watu ambao hawawajibiki kifedha, usishirikiane na watu wa aina hiyo au kuoa/kuolewa nao.
3. Tenga miaka 10 ya kufanya kazi kwa juhudi kubwa sana kujenga kazi/biashara, sifa yako na uhuru wa kifedha.
4. Chagua mtindo wa maisha ambao hauvuki kipato unachoingiza, epuka kuiga mitindo ya maisha ya watu wengine.
5. Weka akiba na wekeza nusu ya kipato chako na wekeza kwenye mifuko ya pamoja yenye gharama nafuu.
6. Kuwa na mpango wa kustaafu na ufanyie kazi mapema.
7. Tumia fursa za uwekezaji ambazo zina kodi ndogo, kama mifuko ya kustaafu.
8. Fanya yote kwa msimamo bila kuacha kwa angalau miaka kumi na utakuwa kwenye njia nzuri ya kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.
9. Usiyumbishwe na kupanda na kushuka kwa soko, hiyo ni hali ya kawaida, kuwa imara na utavuka yote vizuri. Muhimu ni usitaharuki.
10. Unakuwa umefikia uhuru wa kifedha pale unapoweza kuishi kwa kutegemea asilimia 4 ya uwekezaji wako kwa mwaka. Ukifikia hatua hiyo, unaweza kutegemea uwekezaji wako kwa kipindi chote cha maisha yako.
11. Kwa lugha rahisi, uhuru wa kifedha ni pale uwekezaji wako unapokuwa mara 25 ya matumizi yako ya mwaka. Kwa mfano kama matumizi yako ni milioni 1 kwa mwezi, kwa mwaka yanakuwa milioni 12. Unakuwa umefikia uhuru wa kifedha pale thamani ya uwekezaji wako inapokuwa milioni 300 (25 X 12 milioni).
12. Kufikia uhuru wa kifedha haraka, punguza sana matumizi yako.
13. Ukishafikia uhuru wa kifedha, chagua kufanya yale unayopenda kufanya.
14. Mipango yote ya maendeleo unayokuwa nayo, iwekee malengo ya akiba na weka akiba ya kuikamilisha. Epuka kutumia mikopo kwenye mipango ya maendeleo, riba itakurudisha nyuma.
15. Tumia utajiri unaojenga kuwa na mchango mzuri kwa wengine kwa kutoa misaada kwa wale wenye uhitaji.
Hayo ndiyo mambo ya msingi kabisa ambayo mwandishi wa kitabu ameyasisitiza kwa mtu yeyote anayetaka kujenga utajiri na uhuru wa kifedha. Yazingatie ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Kupata mfululizo wa masomo yote ya kitabu THE SIMPLE PATH TO WEALTH, BONYEZA MAANDISHI HAYA.
Tumekuwa na mjadala mzuri wa uchambuzi wa kitabu cha THE SIMPLE PATH TO WEALTH ambapo watu wameshirikisha yale waliyojifunza na hatua wanazochukua. Fungua hapo chini kujifunza zaidi kutoka kwenye kitabu na michango ya wengine.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.
Share this post