Vunja Mzunguko Huu Wa Utajiri Na Umasikini Ili Ujenge Utajiri Wa Kudumu.
Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya vitu vinavyowazuia watu wengi kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni hofu. Na hapa hofu siyo tu ya kukosa au kushindwa, bali pia hofu ya mafanikio. Watu wengi wamekuwa wanahofia kufanikiwa, kwa sababu mafanikio hayo yanawaweka kwenye hatari kubwa ya kushindwa.
Na hofu hiyo siyo ya bure, kwa sababu kuna mifano mingi ya watu ambao walipata mafanikio makubwa, lakini baadaye wakapoteza yote. Wapo wengi ambao walipambana sana na kujenga utajiri mkubwa, lakini wakaishia kuupoteza wote na kurudi kwenye umasikini.
Na hata kwa baadhi ambao waliweza kutunza utajiri wao kwenye kipindi cha maisha yao, baada ya kufa kwao utajiri wao pia haukudumu kwa muda mrefu. Ni mifano hii halisi kabisa imekuwa inawapa watu hofu ya kujenga utajiri na kupata mafanikio makubwa.
Huwa kuna hadithi inayohusu vizazi na utajiri, ambayo inaeleza vizuri mzunguko uliopo kwenye utajiri na umasikini.
Hadithi inaeleza kwamba kizazi cha kwanza huwa kinaanzia kwenye umasikini na hivyo kupambana sana ili kujenga utajiri na kuwa na maisha mazuri.
Kizazi cha pili, ambacho ni watoto wa kizazi cha kwanza wanakuwa wakiwaona wazazi wao wakipambana kujenga utajiri. Hivyo na wao wanaendeleza kujenga utajiri huo ambao wanaupokea kutoka kwa kizazi cha kwanza.
Kizazi cha tatu, ambacho ni watoto wa kizazi cha pili na wajukuu wa kizazi cha kwanza, wanakuwa wamezaliwa kwenye utajiri na hawakuwahi kuyapitia maisha ya umasikini na kuona jinsi juhudi zinahitajika kujenga utajiri. Hivyo kizazi cha tatu huwa kinatawanya utajiri na kuupoteza wote.
Kizazi cha nne kinaanzia kwenye umasikini baada ya kizazi cha tatu kupoteza kila kitu, na hapo mzunguko unaanza upya.
Kwa jamii nyingi, mzunguko huu hauhitaji hata vizazi, kwani unatokea haraka ndani ya maisha ya mtu au muda mfupi baada ya mjengaji wa utajiri kufariki.
Je hii ni laana ambayo haiwezi kuvunjwa?
Habari njema ni kwamba hiyo siyo laana, ni kitu ambacho kinaweza kuvunjwa na utajiri wa kudumu kuweza kujengwa.
Lakini hilo linataka mtu kuanza kufikiria hivyo tangu mapema wakati wa kujenga utajiri, ili kuepuka makosa ambayo yanaweza kumnasa kwenye mitego inayompeleka kwenye mzunguko huo.
Tuchukue mfano wa biashara, ambayo ndiyo njia kuu ya watu kujenga utajiri. Wengi huwa wanaingia kwenye biashara kwa msukumo binafsi, kutokana na mapenzi yao au fursa ambazo wameona. Mwanzoni wao ndiyo wanakuwa watendaji wakuu na kwa sababu wana msukumo mkubwa wa kufanikiwa, wanafanya makubwa sana.
Kwa juhudi kubwa wanazoweka, wanapata matokeo mazuri na biashara inaanza kukua. Hapo panahitajika watu wa kusaidia majukumu mbalimbali na hivyo biashara kuanza kuajiri. Kutokana na ukuaji wa biashara, watu wengi zaidi wanaajiriwa. Lakini pamoja na uwepo wa watu walioajiriwa, bado mmiliki na mwanzilishi wa biashara ndiye mfanyaji mkuu wa maamuzi yote ya biashara hiyo. Asipokuwepo, hakuna kitu kinachoweza kwenda.
Mtu anakuwa amejenga biashara kubwa, ambayo inajiendesha kwa faida, lakini bado inamtegemea yeye. Hata akiweka viongozi, bado mambo mengi yanamtegemea yeye. Mambo huwa yanaenda vizuri pale mtu anapokuwa na afya njema ya kuendelea kuendesha biashara hiyo. Ni pale mtu anapopitia changamoto zinazomzuia kuendesha biashara ndipo anguko kubwa linapotokea. Kwa kuwa biashara haiwezi kwenda bila ya uwepo wake, anapokosekana, biashara inapitia misuko suko na kupata anguko.
Njia pekee ya kuzuia hilo kutokea, ni tangu mwanzo mtu kujenga biashara kwa mfumo sahihi ambapo itaweza kuendelea kwenda hata bila ya uwepo wake yeye. Kwa njia hiyo anaweka miongozo ambayo itahakikisha mambo yote ya msingi yanafanyika na biashara kuendelea kwenda. Pia anaweza kinga ambazo zinazuia biashara hiyo isiathirike na maamuzi mabovu ya baadhi ya watu.
Hayo yote yanawezekana pale mtu unapoamua na kuweka kazi kwenye kujenga utajiri ambao utadumu kwa muda mrefu. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza kwa kina hatua za kuchukua ili uweze kujenga utajiri ambao utadumu. Karibu ujifunze kupitia kipindi hiki ili uvunje huo mzunguko wa utajiri na umasikini ambapo wengi wamenasa.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.