Vigezo Viwili Vya Kufanya Maamuzi Ya Kuingia Kwenye Biashara.
Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye kuingia kwenye biashara, watu wengi huwa wanakuwa na hofu kubwa.
Hofu hiyo inatokana na ukweli mchungu kuhusu biashara, ambao ni uwezekano mkubwa wa kushindwa.
Sehemu kubwa ya biashara mpya zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake.
Hilo linawafanya wale ambao bado hawajaingia kwenye biashara wawe na hofu kubwa ambayo inawakwamisha kwenye kufanya maamuzi.
Ili kurahisisha kufanya maamuzi ya kuingia kwenye biashara, zingatia vigezo hivi viwili; HATARI na UHURU.
Kitu ambacho kinawapa hofu watu kuingia kwenye biashara ni hatari kubwa ya kushindwa ambayo biashara zinayo.
Lakini unapoiangalia hatari hiyo ya kushindwa kwa biashara na hatari zilizopo kwenye njia nyingine za kuingiza kipato, utaona hatari ya biashara ina afadhali.
Tulinganishe biashara na ajira. Wengi huona biashara ni hatari kwa sababu hazina uhakika na kuona ajira ni salama kwa sababu ya uhakika wa kipato.
Tukichimba ndani, utaona ajira ni hatari kuliko biashara. Kwenye ajira una mteja mmoja tu ambaye ni mwajiri anayekulipa. Lakini kwenye biashara una wateja wengi wanaokulipa. Hivyo mteja mmoja akiacha kununua kwenye biashara, unakuwa na nafasi ya kutafuta wateja wengine kabla hujawa kwenye tatizo la kipato. Lakini kwenye ajira, mteja akiacha kununua, ndiyo unakuwa huna kipato kabisa.
Kupunguza hatari ya biashara, toa thamani kubwa ambayo wateja hawaipati na kuwa na wateja wengi zaidi. Kila wakati kazana kuongeza thamani unayoitoa. Na endelea kufikia wateja wapya kila wakati. Ukiweza kufanya hayo mawili, hatari ya biashara inapungua.
Kwenye upande wa UHURU, iko wazi kwamba ajira hazina uhuru, kwa sababu mwajiri anakupangia kila kitu. Kwa bahati mbaya sana, wanaotoka kwenye kuajiriwa, huwa wanaingia kwenye kujiajiri, ambapo nako wanakosa kabisa uhuru kwa sababu wateja wanawapangia maisha. Njia pekee ya kupata uhuru ni kujenga biashara ambayo inaweza kujiendesha bila ya kutegemea uwepo wako wa moja kwa moja.
Hapo tunaendelea kuona jinsi ambavyo maamuzi ya kuigia kwenye biashara ndiyo bora zaidi kwenye shughuli za kujiingizia kipato. Kujenga biashara kunakupa uhuru mkubwa wa kuyaishi maisha yako vile unavyotaka.
Hebu fikiria hapo rafiki, unakuwa na uwezo wa kupunguza sana hatari, wakati huo pia ukiongeza zaidi uhuru wako. Utake nini kingine? Weka juhudi kwenye kujenga biashara ili uweze kupata manufaa hayo mawili.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimeendelea kukufafanulia jinsi ya kutumia HATARI na UHURU kufanya maamuzi bora ya kuingia kwenye biashara. Karibu ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.