Utajiri Ni Utakatifu Na Umasikini Ni Dhambi.
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wawili, waliozaliwa kipindi kimoja, wakasoma shule moja na kuwa na ufaulu mmoja, wanaweza kuanza kazi au biashara ya aina moja kwenye eneo moja. Lakini ukija kuwaangalia baada ya miaka 10, unakuta mmoja amejenga utajiri wakati mwingine yupo kwenye umasikini.
Utashangazwa sana na hali hiyo, iweje watu hao ambao wanafanana kwa mambo mengi ya nje waweze kupata matokeo yanayotofautiana sana kwenye maisha yao?
Na jibu linakuwa ni moja tu, watu hao wanakuwa na mitazamo inayotofautiana kuhusu mambo mengi kwenye maisha. Na moja ya mtazamo wanaokuwa wanatofautiana ni kwenye fedha.
Kiasi cha fedha ambacho mtu anakuwa nacho, huwa kinaanzia kwenye mtazamo anaokuwa nao. Hiyo ina maana kwamba mtu anayekuwa tajiri ni kwa sababu mtazamo wake unakuwa wa kitajiri, wakati mtu anayekuwa masikini mtazamo wake unakuwa ni wa kimasikini.
Mtazamo mbovu sana ambao watu wengi wamejengewa kuhusu fedha ni kwamba utajiri ni dhambi na umasikini ni utakatifu. Mtazamo huu umeanzia kwenye tafsiri isiyo sahihi ya vifungu vya biblia vinavyoeleza ugumu wa matajiri kuingia mbinguni.
Masikini wamekuwa wanatumia mistari ya aina hiyo, na taarifa nyingine zinazowafanya wajione wako vizuri na umasikini wao. Lakini ukweli ni kwamba, umasikini siyo tu ni mbaya, bali pia ni dhambi kubwa sana.
Lengo langu ni kila anayeyapata maarifa ninayoyatoa aweze kujijengea mtazamo sahihi wa mafanikio na utajiri. Mtazamo sahihi utajengwa kwa kuvunja ule mbaya uliopo na kuweka mpya ambao una mchango kwa mtu kufanikiwa.
Tukianza na mtazamo sahihi wa kwamba utajiri ni Utakatifu, ni kwa sababu kupitia utajiri unaweza kufanya mambo mengi mazuri. Unaweza kuwasaidia wale wenye uhitaji, unaweza kutatua changamoto za wengine na unayafurahia maisha.
Umasikini ni dhambi kwa sababu unakuzuia mtu usiweze kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu. Umasikini unakufanya uingie tamaa na wivu kwa wale ambao wamekuzidi kwenye maeneo mbalimbali. Unakuwa masikini kwa sababu unakuwa hujatoa thamani kubwa kwa wengine, na kutokutoa thamani ambayo unawajibika kuitoa hapa duniani, ni dhambi kubwa.
Utasema, lakini matajiri ni wabaya na wana roho mbaya. Siyo kweli. Ukweli ni kuna watu wana roho mbaya, na wanaweza kuwa matajiri au masikini. Masikini akiwa na roho mbaya, hutasikia akisemwa sana, maana madhara yake ni kwa wachache. Tajiri akiwa na roho mbaya utasikia akisemwa sana kwa sababu madhara yake ni kwa wengi.
Mtu kuwa na roho nzuri au mbaya haihusiani na fedha. Ni sawa na kusema watu wenye mikono wana roho mbaya, kwa sababu wanaitumia kuwanyonga watu wengine. Hapo sasa tatizo siyo mikono, bali tatizo ni watu wenyewe. Hivyo tajiri akiwa na roho mbaya, tatizo siyo utajiri, bali tatizo ni mtu mwenyewe.
Fedha huwa inakuza kile ambacho tayari kipo ndani ya mtu. Mtu mwenye roho nzuri akiwa na fedha, hilo litakua zaidi na kuwanufaisha wengi. Mtu mwenye roho mbaya akiwa na fedha, itakuzwa zaidi na kuwadhuru wengi.
Hivyo fedha kama fedha haina tatizo, ni kifaa tu. Tatizo wanalo watu, kwa mitazamo yao na tabia zao.
Je wewe upo tayari kujijengea mtazamo sahihi ambao utakupa utajiri mkubwa kwenye maisha yako? Karibu ujifunze kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini ambapo nimeeleza kwa kina dhana hii ya utajiri ni utakatifu na umasikini ni dhambi. Fungua ujifunze na kuchukua hatua ili uweze kujijengea utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.