UCHAMBUZI WA KITABU; The Rebel (Insha Ya Mtu Aliye Kwenye Uasi)
The Rebel ni kitabu kilichoandikwa na aliyekuwa mwandishi na mwanafalsafa wa Ufaransa Albert Camus. Kitabu hiki kina insha inayoelezea historia na msingi wa kifalsafa wa uasi kwenye bara la Ulaya. Uasi huo umeelezewa kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii kwa ujumla.
Camus amewatumia wanafalsafa na viongozi mbalimbali wa kihistoria kuonesha jinsi hitaji la uasi lilivyojengeka kwa watu na jinsi watu walivyotumia uasi kama njia ya kupinga tawala ambazo hazikuwa za haki na mifumo kandamizi na kufikia ukombozi wa kisiasa, kijamii na kiroho.
Mifumo kandamizi ambayo Camus ameielezea na inayofanya watu kuamua kuasi ni kuanzia kwenye hali binafsi mfano maumivu mpaka kufikia kwenye taifa kwa ujumla kama kupinga tawala za kidikteta. Camus pia ameonesha jinsi sanaa, fasihi na falsafa vilivyoweza kuchangia kwenye vuguvugu la uasi lililokua likiendelea kwenye bara la Ulaya mwanzoni mwa karne ya 20.
Miongoni mwa wale ambao Camus amewatumia kwenye kitabu hiki ni Karl Marx, Friedrich Nietzsche, Georg Wilhelm Friedrich Hegel, Marquis de Sade, Louis Antoine de Saint-Just, Arthur Rimbaud, Mikhail Bakunin, Vladimir Lenin, Sergey Nechayev, Jean-Jacques Rousseau, Adolf Hitler, Max Stirner, André Breton, Ivan Kalyayev, Joseph de Maistre, Comte de Lautréamont, Lucretius, Epicurus, Max Scheler, Fyodor Dostoevsky na Dmitry Pisarev.
Uasi unaanzia kwenye hitaji la watu kutengeneza jamii yenye haki na usawa. Pale watu wanapoona ukosefu wa haki au mifumo kandamizi, wanaona hali haipaswi kuwa hivyo. Wanajua hali inaweza kuwa bora zaidi na watu wakawa na haki sawa na hilo ndiyo linawasukuma kuasi, kukataa mifumo isiyo sahihi na kupigania mifumo sahihi.
Camus anatofautisha uasi (rebellion) na mapinduzi (revolution) kupitia utekelezaji wake na hata matokeo yake. Uasi unaweza kuanza na mtu mmoja au wengi, lakini huwa haujapangiliwa na wala hauwi na ajenda ya kupandikiza mfumo wake. Lakini mapinduzi yanakuwa yamepangiliwa huku yakiwa na ajenga ya kuondoa mfumo uliopo na kuweka mfumo mpya.
Kwa kutumia historia ya mapinduzi mbalimbali, mfano ya Ufaransa yaliyomuondoa Mfalme Louis XVI, Camus anaonesha jinsi mapinduzi yalivyo na madhara na lengo lake ni kuangusha mfumo uliopo ili kuleta mfumo mpya ambao nao hugeuka kuwa kandamizi.
Lengo la mapinduzi ni kuangusha mfumo uliopo na kuleta mfumo mpya bila ya kuangalia manufaa au madhara ya mfumo huo mpya. Lakini lengo la uasi ni kukataa mifumo yote kandamizi, kutaka watu kuwa huru na kuyaishi maisha yao.
Wakati mapinduzi yakiwa kitendo cha kisiasa, uasi ni kitendo cha kiroho pia, kwa sababu kinamuacha mtu akiwa huru na asiyekandamizwa na mfumo wowote.
Wakati Camus anatoa kitabu hiki, mwaka 1951, dunia ilikuwa imepitia changamoto mbalimbali, hasa kwenye nusu ya kwanza ya karne ya 20. Kabla ya kuanza kwa Karne ya 20 dunia ilishuhudia mapinduzi mbalimbali, yakiwepo ya Marekani (1765–1783), Ufaransa (1789–1799), Serbian (1804–1835) na Mapinduzi ya Ulaya kwenye miaka 1820, 1830 na 1848.
Karne ya 20 nayo ikaanza na mapinduzi ya Urusi (1905 – 1907 na 1917), Ujerumani (1918) na mataifa mengine ya Ulaya. Lakini pia hicho ndiyo kipindi ambapo dunia ilipitia vita kuu mbili, ya kwanza (1914–18) na ya pili (1939–45). Katika kipindi hicho pia kuliibuka tawala kandamizi na za kidikteta kama Adolf Hitler wa Ujerumani (1933 – 1945) na Joseph Stalin wa Urusi (1924 – 1953).
Camus alikuwa akijaribu kuyaelewa matukio hayo na kufikia hitimisho kwamba nusu ya kwanza ya karne ya 20 ilikuwa ni kipindi cha watu kuishi kwa hofu, kukandamizwa na mauaji makubwa yaliyoendeshwa na mataifa mbalimbali katika kuanzisha na kupigania itikadi mbalimbali.
Kupitia kitabu hiki na mifano mbalimbali Camus alilenga kuja na njia sahihi ya watu kuweza kuondokana na hali hizo bila ya kutengeneza matatizo zaidi. Kuepuka mapinduzi ya nyumba ambayo yaliondoa mfumo mmoja na kuleta mfumo mwingine ambao ni kandamizi kama ulioondolewa.
Kwenye kitabu hiki pia Camus ameonesha kupitia falsafa yake ya Upuuzi (Absurd) kwamba licha ya watu kutaka maana, dunia haina maana. Anaeleza kwamba uasi wa kweli ni kukataa upuuzi wa ukandamizaji, ukatili na mateso. Muasi anakataa utumwa na ubabe na kusimama kwa ajili ya wengine.
Kwa muasi wa kweli, ukandamizaji na ukosefu wa haki ni vitu visivyovumilika na hivyo anapambana kuleta uhuru na heshima kwa watu wote.
Camus pia amegusia mambo yaliyokuwa ya kawaida katika kipindi hicho, ikiwepo adhabu ya kifo kama ni haki au la.
Kitabu kwa ufupi.
Kwenye utangulizi mwandishi anatueleza nia yake ya kuchunguza hitaji na chanzo cha uasi kwa watu na jamii kwa ujumla. Hapa anahoji iwapo mauaji, yawe ya uhalifu au yanayotolewa kama adhabu ni sahihi.
Kwenye sehemu ya kwanza mwandishi anaelezea maana ya uasi kwa kuangalia aina mbalimbali za uasi na uhusiano wake na historia na mauaji.
Kwenye sehemu ya pili mwandishi anajadili kwa kina uasi wa kiroho na anatumia historia ya Ugiriki, Roma na Biblia kuelezea jinsi roho ya uasi imekuwepo kwa watu. Kwa kutumia hadithi ya kwenye biblia, ya Cain na Abel kuonesha jinsi uasi umeanza zamani.
Kwenye sehemu ya tatu mwandishi anajadili historia ya uasi kwa kutumia mfano wa mapinduzi ya Ufaransa. Anayajadili matukio mbalimbali ya kihistoria na kuonesha jinsi mapinduzi yanavyozalisha hali ambazo ni mbaya zaidi ya zilizokuwepo. Anaangalia pia mapinduzi ya kikomunisti na kuonesha jinsi yanavyotumia hofu na ukandamizaji kuendelea kuwepo, kitu ambacho kinawanyima watu uhuru.
Kwenye sehemu ya nne mwandishi anajadili uasi na sanaa. Hapa anaangalia kazi za wasanii mbalimbali, ikiwepo waandishi na wachoraji na jinsi zilivyochochea roho ya uasi kwa wasanii wenyewe na kwa watu wengine pia. Anaonesha jinsi sanaa ilivyo na nguvu ya kuchochea roho ya uasi.
Kwenye sehemu ya tano, mwandishi anaangalia matumaini ya yale yajayo. Hapa anaangalia yale ambayo dunia ilikuwa imepitia kwenye nusu ya kwanza ya karne ya 21, vita kuu mbili za dunia ambazo zilichochea sana mfumo wa kikomunisti ambao ulikuwa unazidi kuiweka dunia kwenye hatari. Hapa mwandishi anajadili kwa kina iwapo njia zinazotumiwa na mfumo wa kikomunisti kuendelea kutawala ni sahihi au la, mfano mauaji.
Kwenye kuhitimisha kitabu, mwandishi anaonesha matumaini aliyonayo kwenye roho ya uasi, kwamba pale jamii inapokuwa na waasi ambao wanakataa mifumo isiyo sahihi na ambao wana nia njema inasaidia jamii kuwa bora na kuepuka kuanguka kwenye machafuko kama yaliyotokea kwenye nusu ya kwanza ya karne ya 20.
The Rebel ni kitabu kinachotupa msingi wa kusimamia kile kilicho sahihi. Siyo kitabu kinachotufundisha kuwa watukutu au kupindua mifumo iliyopo, bali kinatupa mwongozo wa kusimamia yaliyo sahihi kwa lengo la kuifanya jamii iwe bora zaidi.
Albert Camus amewahi kunukuliwa akisema maisha yako yanapaswa kuwa huru kiasi kwamba kitendo tu cha wewe kuwa hai kinachukuliwa kama uasi. Na hili ndiyo tunakwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, namna tunavyoweza kuishi maisha huru ambayo yatachochea wengine nao kuwa huru na kuondoa kabisa mifumo kandamizi.
Karibu kwenye uchambuzi.
Kitabu kina sehemu tano, kutakuwa na sehemu tatu za uchambuzi kitabu hiki.
Sehemu ya kwanza tunapata utangulizi na sehemu ya kwanza ya maana ya uasi.
Sehemu ya pili itakuwa na uchambuzi wa sehemu ya pili na ya tatu, uasi wa kiroho na historia ya uasi.
Sehemu ya tatu itakuwa na uchambuzi wa sehemu ya nne, tano na hitimisho. Hapo tutajifunza kuhusu uasi na sanaa na matumaini yajayo.
Karibu usome uchambuzi wa kitabu cha THE REBEL ili ujifunze na uweze kusimamia yale yaliyo sahihi kwako na jamii kwa ujumla.
Kupata uchambuzi wa kitabu hicho cha THE REBEL na vitabu vingine vizuri, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.