Tengeneza Pesa Kwa Kutumia Mahusiano.
Rafiki yangu mpendwa,
Kiasili sisi binadamu ni viumbe vya mahusiano kadiri ya vinasaba yaani DNA. Tunahusiana na watu wetu wa karibu kama vile wazazi, wenza, marafiki, jamaa, ndugu na kadhalika. Na asili yetu sisi binadamu ni kupenda kujisikia vizuri pale tunapokuwa kwenye kundi au mahusiano.
Na hata pale tunapokuwa tunahitaji kitu fulani huwa tunaanza kuulizia kwa watu wetu kwa karibu kwanza. Huwa tunawaamini sana watu wetu wa karibu, wale ambao tunahusiana nao. Watu wetu wa karibu pale wanapotupendekezea kitu, huwa tunaondoa hofu kabisa na hivyo kuchukua hatua mara moja bila kusita.
Sina uhakika kama itakufaa lakini vitu vingi ambavyo umenunua, umenunua kwa watu ambao unawajua au wale ambao mnahusiana kwa namna moja au nyingine. Kuna nguvu kubwa sana ya mahusiano katika mchakato mzima wa mauzo.
Kunakuwa na hali fulani ya hofu ndani mwetu pale tunaponunua kitu kwa mtu tusiyomjua. Hapa tunapata picha kwamba, watu wananunua kwa watu wanaowajua, haijalishi unajua nini kwenye maisha yako bali unamjua nani. Watu ambao umejenga nao mtandao, wale ambao unawajua au wanakujua ndiyo watakuwa wa kwanza katika mchakato wa mauzo.
Pata picha katika mahusiano ya kimapenzi, kama umeoa au umeolewa, hujaingia kwenye mahusiano hayo kwa siku moja, bali kulikuwa na mchakato wa muda mrefu mpaka pale mlipoingia katika maisha ya ndoa.
Hata kwenye mchakato wa mauzo, hatuwezi kumuuzia mtu kama hatujajenga naye mahusiano. Watu huwa hawapendi kununua kwa watu wasiowajua, lakini pia watu hawawezi kununua kwa mtu ambaye ameonana naye mara moja tu siku ya kwanza. Kwa mfano, mwanamke akikutana na mwanaume na mwanaume akamtongoza ili awe naye katika mahusiano, katika hali ya kawaida mwanamke hawezi kukubali hapo hapo. Na hata akitokea mwanamke amekubali hapo hapo lazima mwanaume atashtuka na kujiuliza kwa nini nyingi, iweje huyu mwanamke amenikubalia kirahisi hivi? Je, ana kitu gani kilichompelekea anikubali kirahisi?
Kabla ya kumuuzia mteja hakikisha kwanza unajenga naye mahusiano. Ukishakuwa na mahusiano mazuri na mteja basi ni rahisi mteja kununua kwako. Kama mambo yote yakiwa sawa, watu huwa wananunua kwa watu wanaowajua. Je, unamjua nani? Watu wananunua kwa watu ambao wanawajua na ambao wana mahusiano nao. Ukishakuwa na mahusiano yoyote yale na mtu ni rahisi mtu kununua kwako.
Wauzaji wengi wamekuwa na tabia ya kubaka. Yaani wanalazimisha kufanya mauzo kwa mtu ambaye bado hawajajenga naye mahusiano mazuri ambayo yatamshawishi mteja kununua kitu kwao kirahisi. Kabla hujakimbilia kuwauzia wateja wako, jenga nao kwanza mahusiano na wao watakuwa tayari kununua kwako pale wanapokuwa na uhitaji.
Kwenye kila mahusiano ambayo upo, hakikisha watu wanajua unafanya nini. Ili watu waweze kukubaliana na wewe kirahisi kwenye jambo lolote lile kuwa nao kwanza katika mahusiano. Unapokuwa na mahusiano na mteja, mteja anakuona wewe ni rafiki yake na mtu wa karibu na atajisikia vizuri kununua kwako kwa sababu wote mnafahamiana bila shaka.
Watu wakiwa na mambo yao huwa wanaenda kwa watu ambao wanawajua. Hata sisi wenyewe huwa tunapotaka kufanya kitu huwa tunaenda kwa watu tunaowajua. Kwa mfano, hatuwezi kwenda kunyoa kwa kinyozi ambaye hatumjui, hatuwezi kwenda kwa msusi ambaye hatumjui, pale tunapotaka huduma fulani huwa tuko tayari hata kusafiri na kulipa gharama ili kupata huduma kwa wale watu ambao tunawapenda na kuwajali.
Watu wengi wananunua kwa watu ambao wanawapenda. Mtu yuko radhi kulipia gharama kwenda kutafuta huduma mbali hata kama huduma hiyo hiyo ipo karibu naye. Je unafikiri nini ambacho kinampeleka mtu huyo kwenda kutafuta huduma mbali wakati hapo karibu yake ipo? Kwa mfano, watoto wako wanasoma shule ambayo wewe umeipenda na kuwapeleka hapo. Na siyo kwamba hapo unapokaa hakuna shule, mazingira unayokaa yana shule nyingi, lakini kwa nini umeacha hapo na kumpeleka shule ya mbali?
Mauzo Ni Mahusiano.
Kwa sababu watu wananunua kwa watu ambao wanawapenda. Kama watu hawakupendi, hawana mahusiano na wewe wala hata hawatajisumbua kununua kwako. Kabla hujafikiria mauzo, hujafikiria kuuza kile unachotaka kuuza, fikiria kwanza kujenga mahusiano na wale ambao utawauzia kile ambacho unauza au unazalisha.
Katika mahusiano ndiyo mahali ambapo unatengeneza mashabiki wako wa ukweli ambao pale wanapokuwa wana uhitaji wanakuja kwako tu na wala hawamfikiri mtu mwingine ila wewe. Na wale ambao anahusiana nao, wale ambao ni watu wao wa karibu pale wanapokuwa wana uhitaji na kile unachokiuza watawaambia watu wao wa karibu na watakuja kununua kwako.
Mteja akishakuwa na mahusiano mazuri na wewe atakusemea mazuri kwa watu wengine. Na mteja akishakuwa na mahusiano mabaya na wewe atakusemea mabaya. Kulingana na sheria ya 250 ya Joe Girard inasema kwamba kila mtu ana watu 250 ambao anajuana nao moja kwa moja. Hivyo basi, jambo ambalo unafanya kwa mtu mmoja, liwe zuri au baya litawafikia kwa watu wasiopungua 250. Na kama utamfanyia mteja wako kitu kizuri, jua ana nguvu ya kukisambaza kwa watu wengine wasiopungua 250. Na kama utamfanyia mteja wako kitu kibaya jua atakusemea vibaya kwa watu wengine 250.
Kwa mtu yeyote ambaye unahusiana naye, au kwa mteja yeyote ambaye uko naye, usimwangalie kama mtu mmoja, mwangalie kwamba nyuma yake kuna watu zaidi ya 250. Hivyo basi, mauzo ni mahusiano hakikisha unalinda mahusiano yako na wateja ili uendelee kunufaika na mteja wako.
Kitu kimoja zaidi, chukulia mahusiano yako na mteja kama mfuko wa pesheni. Mahusiano uliyonayo na mteja ndiyo yanayowashawishi watu kuja kununua kwako.
Kabla hujaendelea na masomo mengine kwenye kitu hiki cha MAUZO NI MAHUSIANO ondoka na mambo haya kwenye huu utangulizi.
Moja; marafiki wananunua kwa marafiki zao.
Mbili; watu wananunua kwa watu wanaowapenda.
Tatu; ukweli ni kwamba, watu hawanunui kwa watu wasiowapenda.
Nne; watu wanaanza kukununua wewe mwenyewe kwanza na siyo kile unachouza.
Mwisho, mauzo ni mahusiano. Haijalishi unajua nini bali unamjua nani. Kama una changamoto ya mauzo, kitu cha kwanza jiulize unahusiana na nani? Una mahusiano mazuri na wateja wako? Waswahili wanasema, ongea na watu uvae na viatu, hii ina maana kwamba kuwa na mahusiano mazuri na watu nao wao watakuwa tayari kukupa dili nzuri.
Karibu upate kitabu cha MAUZO NI MAHUSIANO ili uweze kujenga mahusiano imara na kufanya mauzo makubwa. Kupata nakala yako ya kitabu, wasiliana na namba 0678 977 007.
Kupata maelezo zaidi ya sura zote za kitabu cha MAUZO NI MAHUSIANO, angalia kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.