Kwa Nini Una 'Aleji' Na Utajiri? Pata Tiba Yake Hapa.
Rafiki yangu mpendwa,
Inapokuja kwenye swala la fedha na utajiri, watu wengi sana ni wanafiki.
Ni wanafiki kwa sababu kwa nje huwa wanajifanya hawapendi kuongelea mambo ya fedha na utajiri. Wakikuona unayaongelea sana mambo hayo wanakuona wewe ni mtu mbaya, mwenye tamaa na usiyejali.
Lakini sasa, watu hao hao, usiku wanakosa usingizi kwa sababu ya fedha. Ni watu wanaokuwa na mahitaji makubwa ya fedha kuliko kipato walichonacho. Wanakuwa na madeni ambayo hawawezi kuyalipa. Wanachelewa kulala kwa sababu ya fedha na wanawahi kuamka kwa sababu ya fedha.
Ni watu wa kutia huruma na kuomba omba wengine wawasaidie pale inapokuja kwenye swala la fedha. Wengi, licha ya kuwa ni watu wazima, wanalazimika kuwanyenyekea hata ambao ni wadogo sana kwao kiumri ili tu wapate fedha, hata kama wadogo hao wanakosea.
Hapo sasa ndiyo unapatwa na mshangao, iweje mtu ambaye pesa inamtesa kwa maisha yake yote, anakuwa mkali kusikia mambo ya fedha?
Ukiwa siyo mwelewa unaweza kuchanganywa sana na hilo. Lakini unapokuja kuwaelewa watu, hasa mazingira waliyokulia na mitazamo waliyojengewa, unaona kwa upande wao wako sahihi kabisa.
SOMA; Kujenga Utajiri Kupitia Usaidizi Na Umaarufu.
Wengi wanakuwa wamekuzwa kwa kujengewa mtazamo kwamba utajiri ni kitu kibaya na matajiri ni watu wabaya. Sasa kwa mtu ambaye miaka 20 ya kwanza ya maisha yake amekuwa anaimbiwa wimbo wa aina hiyo, ataamini hivyo kwa miaka yake yote.
Kwa mtazamo wa aina hiyo, hata mtu anapopata fursa nzuri za kuweza kumpatie fedha na utajiri, anaishia kuzipoteza. Kwa sababu kama kitu hukipendi, huwa kinakukimbia.
Mimi rafiki yako nimejipa wajibu wa kuondoa kabisa huo mtazamo usio sahihi kuhusu fedha kwako. Kila siku lazima nifundishe kitu kuhusu fedha na utajiri. Na hilo limefanya baadhi ya watu kupata makasiriko na mimi kwa sababu naongea sana mambo ya utajiri.
Ni baada ya kuchoshwa na maoni ya wale wanaoona mimi kuongelea utajiri ni kitu kibaya nimeamua kutoa PUVU la kutosha kwa wale wote ambao hawataki kusikia kuhusu fedha na utajiri. Unaweza kupata povu hilo kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini na ukatoka na hasira ya kwenda kupambana ili ujenge utajiri. Nimekueleza wazi kwamba kama unachukia kusikia kuhusu utajiri, usinichukie mimi, maana mimi siyo adui yako, adui yako ni umasikini. Pambana na huyo na mambo yako yataenda vizuri sana.
Pata povu la aleji ya utajiri hapo chini na uchukue hatua sahihi ili uwe na maisha sahihi kwako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.