Jinsi Ya Kuwabadili Watu Unaowaongoza Bila Ya Kuchukiwa Nao.
Rafiki yangu mpendwa,
Kila mmoja wetu ana nafasi ya uongozi kwenye maisha yake. Kama ni kiongozi wa kuchaguliwa au kuteuliwa, unakuwa na watu unaowaongoza. Kama unafanya biashara na umeajiri watu, unawaongoza. Na pia kama una familia, wewe ni kiongozi.
Inapokuja kwenye uongozi, kazi kubwa ni kuwafanya watu wawe tayari kufanya vitu ambavyo hawataki kufanya, lakini vina manufaa kwao. Hilo linahusisha kuwataka watu hao wabadilike, kutoka vile walivyo sasa na kuwa tofauti.
Na hapo ndipo changamoto zote za uongozi zinapoanzia. Kwa asili, watu huwa hawapendi kubadilika na zaidi hawapendi kulazimishwa kubadilishwa na wengine. Mtu yeyote anayewalazimisha watu kubadilika, huwa anaishia kuchukiwa sana na watu hao. Hiyo ni kwa sababu watu wakishakuwa na mazoea yao, huwa wanapenda kuendelea nayo.
Kwa kiongozi hii ni changamoto, kwa sababu hawezi kupata matokeo mazuri anayoyataka kama watu hawatabadilika, na watu ndiyo hao ambao hawataki kubadilika.
Kwa kukosa maarifa sahihi, viongozi wengi wamekuwa wanatumia njia za mabavu na vitisho kulazimisha mabadiliko. Njia hizo ni kuwalazimisha watu wabadilike la sivyo watakosa vitu fulani wanavyovihitaji sana. Mfano kwenye kazi, mtu anaambiwa afanye kitu fulani au la atafukuzwa kazi.
Njia za kulazimisha mabadiliko kwa mabavu na vitisho huwa zinafanya kazi kwa kipindi kifupi, lakini baadaye huwa hazifanyi tena kazi. Watu wanaweza kubadilika ili wasipate adhabu iliyopo, lakini hawatakuwa na ufanisi mkubwa.
Kwenye kitabu cha HOW TO WIN FRIENDS AND INFLUENCE PEOPLE, mwandishi Dale Carnegie ameshirikisha misingi tisa ya kila kiongozi kutumia ili kuweza kuwabadilisha wale anaowaongoza bila ya kuibua chuki. Kwa kuzingatia misingi hii, kiongozi anakuwa na ushawishi mkubwa kwa wale anaowaongoza kubadilika wao wenyewe bila ya kushurutishwa.
Misingi hiyo ni kama ifuatavyo;
1. Anza kwa kusifia na kuthamini kabla ya kuwakosoa watu au kuwaelekeza kile sahihi wanachopaswa kufanya.
2. Waonyeshe watu makosa yao kwa njia isiyo ya moja kwa moja, hii inawapunguzia wao kujitetea na kulinda makosa yao.
3. Ongelea makosa yako kabla ya kuongelea makosa ya wengine, hilo linawafanya wajifunze kwamba kila mtu anakosa na wanaweza kurekebisha.
4. Uliza maswali badala ya kutoa amri au maelekezo, maswali ambayo wanapokujibu wanakuwa wamekubali, ila wanaona wameamua wenyewe na siyo kushurutishwa.
5. Wape wengine nafasi ya kujisitiri hata pale wanapokuwa wamekosea, wasifie watu hadharani, wakosoe faraghani.
6. Wasifie watu kwa kila maboresho wanayofanya, hata kama ni madogo, hilo linawapa shauku ya kuboresha zaidi ili kusifiwa zaidi.
7. Wape watu sifa ambayo watapambana kuitunza mara zote, watu huwa wanapenda kulinda sifa waliyonayo kwa wengine.
8. Watie watu moyo kwa kuwaonyesha makosa waliyofanya ni rahisi kubadili, hilo linawafanya wawe tayari kukiri na kubadili makosa yao.
9. Wafanye watu wajisikie vizuri kufanya kile unachowataka wafanye, kwa kuona kina manufaa kwao na wamehusika kwenye kuamua.
Misingi hii tisa ya kuwa na ushawishi wa kuwafanya watu wabadilike inafanya kazi pale inapofanyiwa kazi na kiongozi wa aina yoyote ile. Katika kuwaongoza na kuwashawishi watu, fanyia kazi misingi hii na utanufaika sana.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA, nimefafanua misingi hiyo tisa pamoja na kutoa mifano ya jinsi unavyoweza kuitumia kama kiongozi na kupata matokeo mazuri. Karibu usikilize kipindi hapo chini na ukayafanyie kazi ili kuwa na ushawishi mkubwa kama kiongozi.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.