Jinsi Ya Kupata Wateja Wengi Kwenye Biashara Yako Kwa Gharama Nafuu.
Rafiki yangu mpendwa katika mafanikio,
Watu wengi wanaoingia kwenye biashara huwa wanajichanganya inapokuja kwenye lengo hasa la biashara. Hudhani lengo la biashara ni kufanya mauzo au kutengeneza faida. Hivyo vyote ni muhimu, lakini ni matokeo ya lengo.
Lengo kuu la biashara yoyote ile ni kutengeneza wateja halafu wateja hao ndiyo wanaoleta mauzo, ambayo yanazalisha faida. Hayo ndiyo maeneo matatu ambayo mfanyabiashara yeyote makini na anayetaka kufanikiwa lazima ayafanyie kazi; WATEJA, MAUZO, FAIDA.
Kwa kuwa mauzo na faida ni matokeo, kwenye wateja ndiyo panapaswa kufanyiwa kazi kubwa, ili basi kazi hiyo kubwa iendelee vizuri kwenye mauzo na faida.
Kupata wateja kwenye biashara huwa kuna gharama, kitu ambacho wafanyabiashara wasiofanikia huwa hawakijui. Wao wanadhani wakishafungua biashara, basi wateja watakuja wenyewe. Hata kama ni kweli wateja watakuja kwa kuwa umefungua biashara, unadhani wamekuja tu? Unadhani kwa nini maeneo ya biashara yaliyopo kwenye mzunguko mkubwa wa watu yana gharama kubwa kuliko yaliyo maeneo yasiyo na mzunguko? Ni kwa sababu maeneo yenye mzunguko unapata wateja wengi zaidi kuliko maeneo yasiyo na mzunguko. Hivyo ongezeko hilo la gharama ni sehemu ya gharama za kupata wateja.
Zipo njia mbalimbali za kupata wateja wapya kwenye biashara, ambazo pia zinatofautiana gharama. Changamoto kwa wafanyabiashara wengi wasiofanikiwa, huwa wanatumia njia ambayo wengine wanatumia, bila kujua kama kwao ina faida au hasara. Kwa sababu njia moja ya kutengeneza wateja haiwezi kufanya kazi sawa kwenye biashara zote.
Kila biashara inapaswa kukokotoa gharama ambazo inaweza kumudu kwenye kupata wateja wapya. Hiki ni kitu ambacho wengi wamekuwa hawafanyi na hilo kuchangia wao kupata hasara licha ya kuwa na wateja wengi.
Kukokotoa gharama za kupata wateja, kunapaswa kuanza na thamani ya maisha ya mteja kwenye biashara. Hii ni jumla ya manunuzi yote ambayo mteja atayafanya kwenye biashara kwa kipindi ambacho atakuwa ananunua.
Tuchukue mfano wa kinyozi, ambaye anatoza Tsh 2,000/= kunyoa, na mteja ananyoa angalau mara moja kila mwezi. Hiyo ina maana kwa mwaka mteja atalipa Tsh 24,000/= na kama atanyoa kwa miaka 10, atalipa Tsh 240,000/=. Hapo bado kuna fursa ya mteja huyo kuleta wateja wengine nao wakawa wananyoa, hivyo thamani yake kuwa kubwa zaidi.
Baada ya kujua thamani ya maisha ya mteja kwenye biashara, unapaswa pia kujua kiasi cha faida ambacho mteja anaingiza kila anaponunua. Kwa mfano huo wa kinyozi, tuseme labda kwenye kila Tsh 2,000/= ya kunyoa, baada ya kuondoa gharama zote, anabaki na Tsh 500/= kama faida.
Kitu cha mwisho kukokotoa ni gharama ya kupata mteja mmoja kwa kila njia ya matangazo unayotumia. Hapa unachukua gharama ambazo zimetumika kufikia wateja na kugawa kwa wateja walionunua. Kwa mfano kama kinyozi ameweka tangazo mtandaoni la kupata wateja na akalipia Tsh 10,000/=, kutoka kwenye tangazo hilo watu 10 wakaja kunyoa, hapo gharama ya kumpata mteja mmoja ni Tsh 1,000/=.
Mpaka sasa tuna hesabu 3; moja ni thamani ya maisha ya mteja, mbili ni faida kwa mteja na tatu ni gharama za kumpata mteja. Hizo ndizo hesabu utakazotumia kufanya maamuzi ya gharama kiasi gani uingie kwenye kupata wateja wapya.
Njia ya kwanza ni kuangalia gharama ambayo ni ndogo au inalingana na faida ya manunuzi ya kwanza ya mteja. Kwa mfano wetu wa kinyozi, kama atapata mteja kwa gharama ya chini ya Tsh 500, bado atakuwa anaenda vizuri.
Njia ya pili ni kutumia njia ambayo gharama yake inazidi faida kwa mteja, lakini kuhakikisha mteja ananunua kwa muda mrefu ili faida kupatikana baadaye. Kwa njia hii unaweza kuingia hasara awali wakati wa kumpata mteja, lakini kwa sababu atanunua muda mrefu, faida itapatikana baadaye.
Njia ya tatu ni kupata hasara kwenye manunuzi ambayo unamvutia nayo mteja, lakini kuingiza faida kwenye mauzo mengine utakayoyafanya anapokuja kwa mara ya kwanza. Kwa mfano wa kinyozi, kama anapata mteja kwa Tsh 1,000/= wakati faida yake ni Tsh 500/=, kama akiweza kumshawishi alipie huduma nyingine anapokuja kunyoa, kama kupakwa dawa kwenye nywele, anarudisha gharama hizo.
Kwa njia hizo unaweza kutengeneza wateja wengi kwenye biashara yako kwa gharama nafuu. Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeeleza hili kwa kina zaidi. Karibu usikilize ili uzielewe vizuri hizo hesabu na ukokotoe kwenye biashara yako na unufaike.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.