Jinsi Ya Kuongeza Uzalishaji Na Ufanisi Wako Kutoka Kitabu The 4 Hour Workweek.
Rafiki yangu mpendwa,
Kila tunachofanya kwenye maisha yetu ni mapambano ya kutoka kwenye umasikini na kujenga utajiri na mafanikio makubwa. Tunapambana kwenye kazi na biashara tunazofanya kwa nia ya kutoka chini na kufika juu zaidi. Pamoja na utajiri na mafanikio, tunataka kuwa na uhuru na maisha yetu.
Lakini kwa bahati mbaya sana, hatua ambazo tumekuwa tunachukua zimekuwa zinatuzuia kupata uhuru. Hata kama tutapata matokeo ya kututoa chini na kwenda juu, tunakuwa tumekosa uhuru ambao ulikuwa ndiyo lengo.
Ndiyo maana unakuta mtu anatoka kwenye ajira, ambayo ilikuwa inampa ukomo wa kipato na kwenda kuanzisha biashara. Kweli biashara inamwezesha kutengeneza kipato kikubwa, lakini inamnyima kabisa maisha. Kwani kadiri biashara inavyokua, ndivyo inavyozidi kutubana kwenye muda na maisha kwa ujumla.
Wajibu wangu ni kuhakikisha wewe rafiki yangu siyo tu unapata utajiri na mafanikio, lakini pia unapata uhuru kamili wa maisha yako. Na ili twende pamoja, tukumbushane uhuru kamili wa maisha maana yake ni nini.
UHURU KAMILI WA MAISHA.
Uhuru kamili wa maisha unaelezewa na vitu vinne;
Moja ni NINI (WHAT) unafanya; hapa unakuwa na uhuru wa kuchagua nini ufanye na nini usifanye. Hulazimiki kufanya kitu chochote kile, ni wewe ndiye unayechagua.
Mbili ni WAKATI (WHEN) unafanya; hapa unatawala muda wako na kuupangilia vile unavyotaka wewe, hulazimiki kuwa mahali popote pale kwa muda fulani.
Tatu ni WAPI (WHERE) unafanyia; hapa unakuwa huru kwenye eneo gani unakuwa, hulazimiki kuwa eneo ambalo hutaki kuwa.
Nne ni NANI (WHOM) unafanya naye; hapa unakuwa na uhuru wa kuchagua watu gani ushirikiane nao na wapi usishirikiane nao. Hulazimiki kufanya kazi au biashara na mtu yeyote ambaye hutaki.
Hayo maeneo manne ndiyo yanayoamua uhuru kamili wa maisha yako. Kama bado unalazimika kufanya yoyote katika hayo manne, haijalishi una utajiri au mafanikio kiasi gani, haupo huru na maisha yako. Na hilo ndiyo la kupambania.
Tim Ferriss, kwenye kitabu chake kinachoitwa THE 4 HOUR WORKWEEK, ametushirikisha jinsi tunavyoweza kupata uhuru kamili wa maisha yetu kwa kutumia kanuni yake anayoiita DEAL.
Kanuni hiyo ya DEAL inasimamia maeneo manne;
Eneo la kwanza ni D (Definition); hapa unayapa mafanikio maana ya tofauti kwako, ambayo inaendana na wewe na siyo kufuata mazoea ya kijamii ambayo yamekuwa kikwazo kwa wengi kupata mafanikio makubwa.
Eneo la pili ni E (Elimination); hapa unaondoa yale ambayo siyo muhimu na hayana tija kwenye maisha yako. Mengi unayohangaika nayo hayana tija yoyote kwenye maisha yako, ukiyaondoa utaweza kujijengea uhuru mkubwa.
Eneo la tatu ni A (Automation); hapa unatumia teknolojia kurahisisha majukumu yote unayoyafanya kwa kujirudia rudia. Sehemu kubwa ya mambo unayofanya kila siku unaweza kutumia teknolojia na ukaokoa muda na nguvu zako.
Eneo la nne ni L (Liberation); hapa ndipo unapata uhuru kamili wa maisha yako ambapo hulazimiki kuwa au kufanya chochote ambacho hutaki wewe. Hapa ndipo unapoyafikia mafanikio kamili ya maisha yako.
Kwa kufanyia kazi maeneo hayo manne kwa uhakika, unaweza kujenga maisha yenye utajiri mkubwa, mafanikio na uhuru kamili.
SOMA; Tabia Saba (07) Za Watu Wenye Ufanisi Mkubwa, Na Wanaofanikiwa Sana.
ONGEZA UTENDANI NA UFANISI ILI KUFANYA MAKUBWA.
Watu wengi huwa wapo ‘bize’ sana, wakiwa wametingwa na mengi wanayofanya, lakini bado hawapati matokeo makubwa. Hiyo ni kwa sababu hawajui kutofautisha kati ya utendaji na ufanisi.
Utendaji ni kufanya kitu vizuri, bila ya kujali ni kitu gani ulichofanya.
Ufanisi ni kufanya vizuri kile ambacho kinakupeleka kwenye malengo yako.
Kwa maana hiyo basi, unachohitaji siyo tu utendaji, bali ufanisi, kwa sababu haina maana kufanya vizuri kitu ambacho hukupaswa kukifanya kabisa.
Ili kuongeza ufanisi, kuna kanuni kubwa mbili unazopaswa kuzielewa na kuzifanyia kazi.
Kanuni ya kwanza ni ya PARETO (80/20) ambayo inasema asilimia 80 ya matokeo unayopata, inatokana na asilimia 20 ya juhudi unazoweka. Maana yake ni matokeo makubwa yanatokana na juhudi zinazowekwa kwenye maeneo machache. Hivyo wajibu wako ni kujua ni maeneo yapi machache ambayo ukiyawekea juhudi zako utapata matokeo makubwa.
Kanuni ya pili ni PARKINSON ambayo inasema jukumu huwa linachukua muda ambao limetengewa kufanyika. Ikiwa na maana kwamba kwa jukumu lile lile, ukilitengea muda mrefu litakamilika kwenye muda huo na hata ukilitengea muda mfupi litakamilika kwenye muda huo. Na hapa wajibu wako ni kutenga muda mfupi kwa ajili ya kukamilisha majukumu muhimu ili uweke umakini wako na kuyakamilisha.
Sasa basi, ukitaka kuwa wa moto sana na uweze kufanya makubwa ndani ya muda mfupi, chagua yale majukumu ya muhimu zaidi kuliko mengine yote, halafu panga kuyafanya ndani ya muda mfupi.
Swali muhimu ambalo unapaswa kujiuliza kila siku na kupambana kulifanyia kazi ni hili; Kama unaruhusiwa kufanya mambo mawili tu kwa siku na kuyafanya ndani ya masaa mawili tu, je ni nini ungefanya? Jiulize swali hili na hakikisha unajipa majibu sahihi na hayo ndiyo unapaswa kuyafanyia kazi.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA tumekuwa na mjadala wa masoko kutoka kitabu hicho cha THE 4 HOUR WORK WEEK, karibu ufungue kipindi hapo chini na kujifunza ili uweze kuwa bora na kupata uhuru kamili wa maisha yako.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.