Jinsi Ya Kukabiliana Na Magumu Ya Maisha Kwa Kutumia Falsafa Ya Ustoa.
Rafiki yangu mpendwa,
Magumu na changamoto za maisha ni vitu ambavyo haviwezi kuondoka kabisa. Pale tu tunapokuwa hai, tunakutana na mambo mbalimbali ambayo ni tofauti na tulivyokuwa tunatarajia.
Watu wengi wamekuwa wanakata tamaa kwenye maisha kwa sababu ya kuwa na matarajio yasiyo sahihi. Wengi wanapokuwa wanaanzia chini na kukabiliwa na magumu na changamoto, wanaamini wakipambana na kufanikiwa basi hawatakuwa tena na magumu hayo. Ni pale wanapopambana na kufanikiwa na kugundua magumu na changamoto bado vipo, vinakuwa tu vimebadilika.
Hivyo basi, badala ya kupuuza hayo magumu na changamoto, au kutamani visingekuwepo kabisa, tunapaswa kujifunza namna bora ya kukabiliana nayo ili tuweze kuwa na maisha tulivu.
Aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa, Marcus Aurelius, kwenye kitabu chake cha nne cha Meditations aliandika mambo muhimu sana ya kuzingatia ili tuweze kukabiliana na magumu na changamoto za maisha.
Wazo kubwa sana ambalo amelielezea kwenye kitabu hicho na ambalo kila mtu anapaswa kulielewa na kulifanyia kazi ni hili; DUNIA NI MABADILIKO NA MAISHA NI MAONI.
DUNIA NI MABADILIKO.
Sehemu ya kwanza ya dhana hiyo kuu ya kukabiliana na magumu Kistoa ni kujua kwamba dunia ni mabadiliko. Hiyo ina maana kwamba kila kitu kwenye dunia kinabadilika, hakuna chochote kinachobaki kama kilivyo.
Hili ni jambo muhimu sana ambalo wote tunapaswa kulielewa na kuliishi, kwa sababu huwa tunayakuza magumu kama vile yanadumu milele. Hakuna magumu au changamoto zozote zinazoweza kudumu milele. Zitafika mahali na kubadilika au wewe hautakuwepo tena.
Hivyo haijalishi unapitia nini, jua muda ni mwalimu na tiba nzuri. Kadiri muda unavyokwenda mambo hayo yatabadilika, au yataondoka kabisa. Na kama hayataondoka, basi wewe utaondoka na kuyaacha.
Je kuna haja ya wewe kusumbuka na chochote ili hali mabadiliko yatakuja? Kuna haja ya wewe kukata tamaa wakati hakuna kinachobaki vile kilivyo milele? Ni dhahiri kwamba yote hayo hayana haja, wajibu wako ni kukabiliana na yale unayokutana nayo kwa namna sahihi, ukijua hayatadumu milele.
Kamwe usikate tamaa na kuona chochote unachokutana nacho ndiyo mwisho, kila kitu kinabadilika, anza kwa wewe kubadilika na kuwa tayari kupokea mabadiliko ya vitu vingine ili kunufaika navyo.
MAISHA NI MAONI.
Sehemu ya pili ya dhana ya kukabiliana na magumu Kistoa ni kujua kwamba kila kitu tunachojua na kufikiria kuhusu maisha ni maoni yetu wenyewe. Huwa hatuoni vitu kwa jinsi vilivyo, bali kwa namna tulivyo sisi wenyewe. Jinsi tunavyoyaona maisha inaathiriwa sana na mtazamo ambao tunakuwa nao.
Na hili ni kweli kabisa, hasa ukifikiria mambo ambayo umewahi kusumbuka nayo sana, ukihofia yatakapotokea yatakuwa na madhara makubwa, lakini yalitokea na madhara hayakuwa kama ulivyofikiria. Mambo mengi sana tunayofikiria na kuchukulia sivyo yalivyo kwenye uhalisia.
Hivyo katika kukabiliana na magumu na changamoto za maisha tunapaswa kuwa watulivu sana na kuhakikisha tunakiangalia kitu kama kilivyo kwa uhalisia wake. Hili linatutaka tujilazimishe kuvunja mitazamo ambayo tayari tunayo na inakuwa kikwazo kwetu.
Kwa kujilazimisha uone kila kitu kwa jinsi kilivyo, kwa uhalisia wake, utaondoa mengi ambayo yanapelekea utengeneze tafsiri zisizokuwa sahihi kwenye vitu. Na hili unapaswa kujikumbusha kila mara, hasa pale unapohukumu kitu haraka kabla hujakitafakari kwa kina.
Kuna mengine ambayo Marcus Ameyashirikisha kwenye kitabu hicho, kama msimamo kwamba hakuna chochote nje ya fikra zako ambacho kina nguvu kwako. Ni kile unachokiruhusu ndiyo kinachoweza kukuathiri. Hili pia lina nguvu sana kwenye kukabiliana na makubwa kwenye maisha yako.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA nimeshirikisha kwa kina jinsi ya kutumia falsafa ya Ustoa kuweza kukabiliana na magumu na changamoto za maisha, karibu ujifunze kwenye kipindi hiki na uweze kuwa bora.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.