Jinsi Ya Kujenga Utajiri Wa Mwendokasi.
Rafiki yangu mpendwa,
Utajiri ni kitu kizuri sana kwenye maisha.
Hiyo ni kwa sababu utajiri unatuweka huru, kwa kutuwezesha kuyaishi maisha yetu vile tunavyotaka.
Kitu kimoja ambacho watu wengi huwa hawakijui ni kwamba kila mtu anaweza kuwa tajiri. Ndiyo, namaanisha kila mtu kabisa, ikiwepo wewe mwenyewe.
Haijalishi uko kwenye hali gani au unafanya shughuli gani, uwezo wa kujenga utajiri mkubwa upo ndani yako kabisa.
Na hata kama umeshafanya makosa mengi na kupoteza muda, bado ule uwezo wa kujenga utajiri mkubwa upo ndani yako. Ni wewe tu uamue kuanza kuutumia uwezo huo na kunufaika nao.
Rafiki, njia ya kujenga utajiri imegawanyika kwenye pande mbili.
Upande wa kwanza ni njia ya mwendo wa pole. Hii ni njia ambayo mtu yeyote anaweza kuitumia bila hata ya kujisukuma sana. Yaani anachohitaji ni kuweka tu mpango na kisha kuufuata kwa muda. Hahitaji kusumbuka na kitu kingine chochote.
Njia hii ina kanuni rahisi tu ambayo ni WEKEZA ASILIMIA 10 YA KIPATO CHAKO KWA MUDA MREFU BILA KUACHA. Ni hivyo tu rafiki, kwa kila kipato unachoingiza, unawekeza asilimia 10 na kusahau. Unaenda hivyo kwa msimamo bila kuacha.
Kwa njia hii ya mwendo wa pole, inakuchukua miaka 20 mpaka 30 kujenga utajiri, kulingana na ukubwa wa kipato chako na matumizi yako.
Njia hii inawafaa sana wale ambao ndiyo kwanza wanaanza shughuli zao za kuingiza kipato na umri haujaenda sana. Wenye miaka 20 mpaka 40 wanaweza kutumia njia hii na wakafikia utajiri kwa uhakika kwenye maisha yao.
Kuna wale ambao wanaona miaka 20 mpaka 30 ni mingi na huenda umri umekwenda, labda wana miaka zaidi ya 50. Japo njia ya mwendo wa pole inawezekana katika kipindi chochote, kama unataka zaidi, ipo njia nyingine.
Na hiyo ni njia ya mwendokasi. Njia ya mwendokasi kwenye kujenga utajiri inachukua miaka 10 mpaka 15 kufikia utajiri. Njia hii inamfaa mtu yeyote, lakini inahitaji kazi ya ziada kuliko njia ya mwendopole ambayo tumeshaiona.
Kwenye njia ya mwendokasi wa kujenga utajiri, unawekea nusu ya kipato chote unachoingiza. Na hapo ndipo kazi yake kubwa ilipo. Yaani unapaswa uweze kuishi kwenye nusu ya kipato chako. Mahitaji yako yote ya maisha yasizidi nusu ya kipato, ili nusu inayobaki ndiyo unaiwekeza.
Ukiweza kuwekeza nusu ya kipato chako, inakuchukua kati ya miaka 10 mpaka 15 kufikia utajiri na uhuru wa kifedha. Njia hii inachukua muda mfupi kwa sababu kiasi cha uwekezaji unachofanya ni kikubwa, hivyo utajiri unajijenga kwa kasi. Wakati huo huo gharama za maisha yako zinakuwa ndogo, hivyo kufikisha uwekezaji wa kukutosha kuendesha maisha yako haichukui muda mrefu.
SOMA; Hatua Tano Za Kutoka Kwenye Madeni Yanayokukwamisha Kujenga Utajiri.
Ili kuweza kufanyia kazi njia ya mwendokasi wa kujenga utajiri, unahitaji kufanya vitu viwili;
Kitu cha kwanza ni kupunguza sana gharama za maisha yako. Hapa unaondoa matumizi yote ambayo siyo ya msingi ili uweze kuwekeza nusu ya kipato chako. Hii inaweza isitoshe, kwa sababu kuna gharama huwezi kuziondoa.
Kitu cha pili ni kuongeza sana kipato chako. Hapa unakuza kipato unachoingiza ili uweze kufanya uwekezaji ambao ni mkubwa zaidi. Kwa wale ambao kupunguza kipato bado hakutoshi kuwekeza nusu, kuongeza kipato ni lazima.
Ili kuhakikisha hukwami kwa namna yoyote, unapaswa kufanyia kazi njia zote mbili kwa pamoja. Unapunguza sana gharama za maisha yako, huku ukiongeza zaidi kipato chako. Ukifanya yote mawili kwa pamoja, kufikia utajiri na uhuru wa kifedha linakuwa jambo la haraka na uhakika.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimefafanua kwa kina jinsi unavyoweza kutumia njia ya mwendokasi kujenga utajiri wa uhakika kwenye maisha yako. Fungua ujifunze.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.