Fanya Mambo Haya Mawili (2) Kama Unataka Kujenga Biashara Yenye Mafanikio Makubwa.
Rafiki yangu mpendwa,
Njia ya uhakika ya kujenga utajiri mkubwa ni kuwa na biashara kubwa, ambayo inajiendesha yenyewe bila ya kukutegemea wewe moja kwa moja.
Watu wengi wanaoingia kwenye biashara huwa wanashindwa kujenga biashara zenye ukubwa wa aina hiyo. Wanaishia kujitengenezea ajira zao binafsi ambazo zinawategemea muda wote.
Kama biashara unayoifanya inategemea uwepo wako ndiyo iweze kwenda, basi hiyo siyo biashara bali ni ajira binafsi. Haiwezi kupata aina ya ukuaji utakaoweza kukupa utajiri mkubwa.
Ni wachache sana ambao wamekuwa wanafanikisha kujenga biashara kubwa kiasi cha kuwapa utajiri mkubwa. Wengi wamekuwa wanaishia kuwa na biashara ndogo ambazo nyingi huishia kufa kutokana na kushindwa kuendelea pale mtu anapokuwa hayupo.
Kinachotofautisha biashara zinazokuwa kubwa na zile zinazobaki kwenye udogo siyo aina ya biashara, wala siyo hali ya uchumi. Kwenye kila aina ya biashara kuna kubwa na ndogo na kwenye kila aina ya uchumi kuba biashara zinazofanya vizuri na zinazoshindwa.
Kama biashara itakuwa kubwa na kumpa utajiri au kama itabaki kuwa ndogo, inaanza na mmiliki wa biashara. Mmiliki wa biashara ndiye anayeamua biashara iwe kubwa kiasi gani. Na anafanya hivyo kwa njia kuu mbili.
Njia ya kwanza ni kwa namna anavyofikiri. Hapa inaanzia kwenye malengo ambayo mtu anakuwa nayo na kuyasimamia wakati wote. Wasikilize wengi kwa nini wapo kwenye biashara na utasikia wakisema wanataka kupata hela ya kula. Je unadhani nini kitatokea wakishapata hela ya kula?
Wale wanaojenga biashara kubwa na zinazowapa utajiri, huwa wana malengo makubwa kwenye biashara hizo. Wanakuwa na msukumo wa kufanya makubwa na siyo tu kupata fedha za kuendesha maisha. Malengo makubwa wanayokuwa nayo ndiyo yanawafanya waweze kuona na kutumia fursa kubwa zilizopo na kupata matokeo ya tofauti.
Njia ya pili ni namna ya kufanya. Hapa inahusisha hatua ambazo watu wanachukua kwenye kujenga biashara zao. Wale wanaobaki na biashara ndogo, huwa wanafanya biashara zao kwa mazoea sana. Wanafanya yale ambayo wamezoea kufanya na kuishia kupata matokeo ambayo huwa wanayapata. Kwa kuchukua hatua za kawaida na tena kwa mazoea, wanashindwa kufanya makubwa.
Wanaojenga biashara kubwa na zenye mafanikio huwa wanachukua hatua kubwa sana kwenye ujengaji wa biashara zao. Wanachukua hatua za tofauti na ambazo zinaendelea kuboreshwa kulingana na matokeo yanayopatikana. Ni kupitia kuchukua hatua ambazo ni kubwa ndiyo matokeo makubwa pia yanavyozalishwa.
Kwa kuleta pamoja kufikiri kwa ukubwa, kwa kuwa na malengo makubwa na kufanya kwa ukubwa, kwa kuchukua hatua kubwa sana ndiyo biashara kubwa zinavyojengwa, biashara ambazo zinawapa watu utajiri na uhuru kamili wa maisha yao.
Grant Cardone, mwandishi, mkufunzi wa mauzo na mwekezaji kwenye majengo, kwenye kitabu chake cha 10X Rule anashirikisha hadithi ya jinsi alivyoweka malengo makubwa na kuyapambania kwa ukubwa. Katika kuhakikisha anawafikia watu wengi zaidi kwenye huduma zake, Grant alijiwekea lengo la kujulikana na watu wote duniani. Hilo lilikuwa lengo kubwa sana ambalo hajawahi kuwa nalo wala hajawahi kulisikia popote.
Ili kufikia lengo hilo kubwa, Grant aliweka mipango ya hatua za kuchukua, ambazo kwa sehemu kubwa ilikuwa ni kuonekana na wengi zaidi, kupitia vipindi vya TV na mitandao ya kijamii. Lakini kulikuwa na tatizo moja, hakuwa anajulikana sana na hilo kuwa kikwazo kwake kupata vipindi vya TV, kwa sababu vimekuwa vinatolewa kwa wale ambao tayari wana umaarufu.
Kwa kutumia misingi ambayo amefundisha kwenye kitabu cha 10X, Grant aliweza kulifanikisha hilo. Nimeshirikisha hadithi hiyo ya Grant kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini. Fungua uweze kujifunza ili na wewe ujenge biashara kubwa na inayokupa mafanikio.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
0678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.