Fanya Hivi Kudumu Na Wateja Wa Biashara Yako Milele.
Rafiki yangu mpendwa,
Huduma ni shughuli inayofanywa kwa manufaa ya mtu au watu wengine. Mfano, hospitali kuna huduma ya kwanza anayopewa mgonjwa baada ya kupata majeruhi. Shuleni kuna huduma ya mafunzo kwa wanafunzi, ili wapate uelewa zaidi. Kwenye usafiri mfano ndege, kuna huduma ya vinywaji na maelekezo kabla, wakati na baada ya safari. Kwenye mitandao ya simu kuna huduma ya kutatuliwa changamoto za mawasiliano na nyingine. Kwenye benki kuna huduma ya ushauri wa kifedha na maelekezo namna ya kufungua akaunti.
Mhudumiaji ni mfanyakazi anayetoa huduma kwa mteja. Inaweza kuwa huduma ya moja kwa moja kumuonyesha au kwa njia ya mazungumzo ya simu. Ambapo hutoa ufafanuzi kuhusu jambo fulani linalomtatiza mteja. Mteja anapokutana na mhudumiaji anakuwa huru kuongea na kuuliza chochote, huku akipewa majibu sahihi ya kile anachouliza.
Kwenye mauzo mhudumiaji kazi yake kuu ni kuwabakiza wateja, kuwafanyia mauzo ya ziada na kupata wateja wa rufaa. Maana kupitia uhudumiaji mteja anatatuliwa changamoto anazokuwa nazo. Wahudumiaji ndio huwafanya wateja kuifurahia huduma inayotolewa na kampuni, taasisi au ofisi husika.
Sifa kuu ya mhudumiaji lazima awe ana uzoefu au anaijua biashara au huduma kwa kina zinazotolewa na ofisi, kampuni au taasisi husika. Ni jambo la kushangaza pale mteja anauliza kitu fulani mhudumiaji anaanza kubabaika bila kujua kitu cha kufanya. Sifa nyingine, ni pamoja na kuwajua wafanyakazi wenzake na majukumu yao. Hii inamrahisishia kazi, linapotokea jambo lililo juu yake apate urahisi kumuelekeza mteja na mwishowe apate utatuzi.
Tunaposema huduma kwa wateja, tunamaanisha wewe unayewahudumia wateja upekee wako upo kwenye neno HUDUMA. Watu wote wanaweza kupata wateja na kuwahudumia. Ila kinachofanya wateja kuja kwako ni upekee wa huduma unayotoa. Kuanzia kwenye kumpokea mteja, kuongea naye, kumjibu, kumpatia bidhaa, kumfuatilia au kumjulia hali. Huduma ikiwa zaidi ya matarajio yake lazima mteja apate furaha.
Watu wengi wamekuwa wanadhani huduma kwa wateja ni kitu kinachotolewa na taasisi, kampuni, ofisi au watu maalumu. Hii sio kweli. Kila mmoja anatoa huduma kwa wateja kulingana na kitu anachofanya. Kama wewe ni mwalimu, jua unatoa huduma kwa wanafunzi. Wanafunzi ndio wateja wako. Bila wao kazi yako haiwezi kuwa na ufanisi. Ni kupitia wanafunzi unapata malipo yako.
Daktari wa binadamu unawahudumia wagonjwa. Wagonjwa ndio wateja wako. Bila wao kuja katika sehemu yako kupata huduma ya matibabu, kazi yako isingekuwa na ufanisi wowote. Maana, huwezi kwenda kutibu magari au miti. Utaalamu wako upo kwenye kuwatibu watu. Kupitia wagonjwa ndipo unapata malipo yako.
Dereva unayeendesha gari, usiseme mimi siwezi kutoa huduma kwa wateja. Utakuwa unakosea. Abiria ndio wateja wako. Ikiwa utawaheshimu, kuwasikiliza na kuwasaidia, kazi yako itakuwa na ufanisi mkubwa. Watu wanapenda kuwaambia wengine jinsi gani umewafanya wajisikie vizuri. Ni kupitia nauli zao malipo yako yanapatikana.
Mama Ntilie unayeuza chakula, usiseme mimi sipo upande wa huduma. Kuuza kwako chakula tayari ni huduma tosha. Unawasaidia watu wenye njaa kupata chakula. Kupitia malipo yao unapata pesa. Pesa hiyo inakusaidia kukuza mtaji wako. Kesho unapanua kibanda chako na kuajiri wahudumiaji wengine. Hivyo, na wewe ni sehemu ya watoa huduma kwa wateja.
Ndugu yangu mpendwa, huduma kwa wateja inatolewa katika kila eneo la maisha yako. Usijifungie eneo moja kwamba, huduma inatolewa kwa watu wenye biashara, taasisi za kifedha au simu tu.
SOMA; Jinsi Ya Kuwafanya Watu Wakubaliane Na Mawazo Yako Kanuni Ya Kumi
Kila eneo la maisha yako linafaa kutoa huduma. Maana umezungukwa na watu. Kupitia watu hao hao ndio unapata pesa na fursa mbalimbali za kufanya vitu vingine. Sehemu ya biashara ndiyo huduma kwa wateja inafanya kazi zaidi. Maana ndipo mzunguko mkubwa wa watu ulipo. Na wengi wetu tulishazoeshwa hivyo kwamba, huduma kwa wateja ipo tu kwenye biashara.
Uzuri ni kwamba kila mtu ni muuzaji. Kama nilivyosema hapo awali, kama wewe ni rasilimali watu, unauza muda na ujuzi wako kwenye kampuni. Una genge au duka unauza bidhaa kwa mteja. Ukiielewa dhana hii itakusaidia kwa kila mtu unayekutana naye kwenda naye sambamba, ili akuunganishe na watu wengine zaidi.
Tunapozungumzia suala la huduma kwa wateja, tunagusia eneo muhimu katika kuwahudumia wateja. Kwa sasa karibia taasisi zote kubwa zinatoa huduma kwa wateja. Mara nyingi ni kupitia kitengo cha huduma kwa wateja (customer service center). Kitengo hiki kinahusika kuwasikiliza wateja na changamoto zao. Huduma hizi hutolewa kulingana na ukubwa wa taasisi. Wapo wanaotoa masaa ishirini na nne na wapo wanaotoa masaa kumi na mbili.
Huduma kwa wateja ni sehemu muhimu ya kutoa thamani kwa mteja katika biashara yako. Unachopaswa kujua ni kwamba; “wateja wana kumbukumbu. Watakukumbuka wewe, uwe unawakumbuka au la”. Zaidi imani ya mteja inaweza kuharibiwa mara moja na tatizo kubwa la huduma au inaweza kuhujumiwa siku kwa siku, kwa makosa madogo madogo yanayojitokeza mara nyingi katika uhudumiaji.
Biashara yoyote ile inahitaji watu waliokusudia kutoa huduma nzuri kwa wateja. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wateja ndiyo nguzo kuu ya biashara ambazo mtu anafanya. Ndiyo maana tuna msemo maarufu wa Kiswahili usemao, “Mteja ni mfalme”. Huu sio msemo wa kujifariji, hapana. Ipo maana kubwa ndani yake. Maana kupitia mteja ndipo biashara inapata pesa za kujiendesha.
Ni kutokana na msingi huu wa mteja ni mfalme, uliosababisha kampuni kubwa zinakuwa na kitengo cha huduma kwa wateja. Mara nyingi kitengo cha huduma kwa wateja huwa kina watu waliosomea au walio na uzoefu wa namna ya kuwahudumia wateja vizuri.
Kwa chochote kile unachofanya, kuna namna unawagusa watu wengine. Ili uweze kuwa na ushawishi mzuri kwa wale unaowagusa kwenye hicho unachofanya, unapaswa kuwapa huduma nzuri sana.
Ni pale unapowapa watu huduma ambayo hawawezi kuipata mahali pengine ndiyo wanakuwa tayari kurudi kwako zaidi na zaidi. Na hapo unakuwa umewateka watu hao milele.
Ili uweze kutoa huduma bora kwa wale unaowagusa na kubaki nao milele, pata na usome kitabu cha MAUZO NI HUDUMA. Kitabu hiki kinakueleza hatua kwa hatua yote unayopaswa kufanya ili kuwahudumia vizuri wale unaowalenga na kudumu nao.
Kupata nakala ya kitabu cha MAUZO NI HUDUMA, wasiliana na namba 0678 977 007.
Kwenye kipindi cha ONGEA NA KOCHA hapo chini nimekupitisha kwenye masomo 10 yaliyopo kwenye kitabu hicho cha MAUZO NI HUDUMA. Fungua kipindi hicho upate mwanga wa manufaa makubwa yaliyo kwenye kitabu hicho na kuchukua hatua mara moja.
Nenda kayaweke haya uliyojifunza kwenye matendo ili uweze kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kuiishi kila siku yako kwa mafanikio makubwa.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani,
Daktari |Mwandishi |Kocha |Mkufunzi
+255 678 977 007 / amakirita@gmail.com
MUHIMU; Rafiki, nikushukuru kwa kuendelea pamoja kupitia mafunzo haya ninayotoa. Karibu kwenye huduma zaidi ninazotoa, kuanzia 1. VITABU, 2. NGUVU YA BUKU, 3. KISIMA CHA MAARIFA, 4. CHUO CHA MAUZO na 5. BILIONEA MAFUNZONI. Kupata maelezo ya huduma hizi, tumia mawasiliano yaliyopo hapo juu. Karibu sana.